25/10/2025
RDO WAHAMASISHA VIJANA KUPIGA KURA OCTOBER 29....
Shirika la Maendeleo (RDO) limeendelea kuonesha uzalendo na kujitolea katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi, hususan vijana, katika masuala ya kitaifa hasa katika uchaguzi mkuu unaofanyika Jumatano ya Oktoba 29.
Kupitia ufadhili wao RDO kwa mashirika la MMADEA na Action for Change yaliyopewa kibali cha kutoa elimu ya Mpiga kura na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Oktoba 23 wametoa elimu ya Mpiga kura kwa vijana wa Vyuo vya ufundi vilivyopo mjini Mafinga, kuelekea uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na rais, katika ukumbi wa chuo cha Ufundi Lutherani kilichopo Mji Mafinga mkoani Iringa.
Vyuo hivyo vya Mafunzo na Ufundi stadi vilivyoshiriki ni Pamoja na Chuo cha RDO Mafinga, chuo cha Mafunzo NAJA, Chuo cha Misitu na bidhaa za misitu (Fwitic) Pamoja na Chuo cha Mafunzo Lutherani (Mwenyeji).
Akizungumza Mratibu wa Vyuo vya RDO Tanzania Ndg. Obadia Ngailo amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo vijana na kuwapa uelewa sahihi kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu, ikizingatiwa kuwa wengi wao tayari wana sifa za kupiga kura katika uchaguzi huu.
Naye Mkufunzi wa mafunzo hayo, Ndg. Raphael Mtitu ambaye ni Mkurugenzi wa shirika la MMADEA linaloendesha hughuli zake mkoani Iringa, na Renatus Mpiluka ambaye ni Mratibu wa Shirika la Action for Change wamewahimiza vijana kujitokeza kuchagua viongozi wanaowataka badala ya kuwaachia wengine kufanya maamuzi kwa niaba yao.