15/07/2025
INEC YAENDESHA MAFUNZO KWA WATENDAJI WA UCHAGUZI KATIKA MIKOA YA MTWARA NA LINDI
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetoa mafunzo kwa Waratibu wa Uchaguzi wa Mikoa, Wasimamizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi, ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi na Maafisa Ununuzi kutoka Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Mafunzo hayo ambayo yameenda sambamba na washiriki kula kiapo cha uaminifu, yanafanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa Benki Kuu Tanzania tawi la Mtwara, kuanzia leo Tarehe 15-17 Julai 2025.
Ufunguzi wa mafunzo hayo umefanywa na Mhe.Balozi Omari Ramadhani Mapuri ambaye ni Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, aliyesisitiza juu ya washiriki kuzingatia weledi wakati wote watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
"Napenda kuwakumbusha kuwa uteuzi wenu umezingatia uaminifu,uadilifu,uzalendo, kwa kuzingatia haya mmeteuliwa kwa mujibu wa sheria kusimia uendeshaji wa uchaguzi katika maeneo yenu ya uchaguzi "
"Dhamana mliyopewa ni kubwa,nyeti na muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu hivyo Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inayo imani kuwa mtasimiamia vema zoezi hili hadi litakapokamilika"
Kuhusu ushiriki wa wadau, Balozi Omari Mapuri amesisitiza juu ya wasimamizi hao kuwashirikisha wadau wote uchaguzi, vikiwepo vyama vya siasa katika kila hatua inayowataka kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
Awali Mhe.Bozi Omari akiwa na watendaji wengine wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, walitembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, ambapo walikuna na mwenyeji wao Kanali Patrick Sawala.
Mafunzo hayo pia yanaendelea katika mikoa mbalimbali nchini, kwa lengo la kuhakikisha kuwa wasimamizi wa uchaguzi wanafikiwa na elimu ya kutosha kabla ya kuanza mchakato wa uchaguzi.
Awali mafunzo hayo yalitanguliwa na Watendaji hao wa Uchaguzi kula kiapo, kilichoongozwa na Mhe.Hakimu Allex Kalagaza Robert.
✍️ Bryson Mshana