15/07/2026
*NAIBU SPIKA SILLO AUNGANA NA WANANCHI MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU.*
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, ameungana na wananchi kuupokea Mwenge wa Uhuru uliowasili leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati ukitokea Wilaya ya Kiteto.
Akizungumza mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang'onda, Sillo amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kupeleka fedha nyingi katika Jimbo la Babati Vijijini kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi.
Amesema uwekezaji huo umewezesha utekelezaji wa miradi katika sekta muhimu zikiwemo elimu, afya, maji, barabara na huduma nyingine za kijamii, hatua ambayo imeendelea kuharakisha maendeleo ya wananchi wa wilaya hiyo.
Sillo amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda na kutunza miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang'onda, ameendelea na ratiba ya kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati.
Kaulimbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 inasema: "Tanzania ni Yetu Sote, Tushik**ane kwa Pamoja Kuleta Maendeleo."