
30/07/2025
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema Mkoa huo unaandika historia mpya kupitia uzinduzi wa Bandari Kavu ya Kwala na miradi mingine mikubwa ya kimkakati itakayofanyika Julai 31, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 30, 2025 katika eneo la tukio, Kunenge alieleza ,maandalizi ya hafla hiyo yamekamilika na amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo la kihistoria.
“Tunaweka historia mpya mkoani Pwani, Huu ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kujenga uchumi wa viwanda na kuimarisha miundombinu ya kisasa,” alieleza Kunenge.
Alieleza Rais Samia atazindua Bandari Kavu ya Kwala, safari ya treni ya mizigo kupitia reli ya kisasa (SGR), mapokezi ya mabehewa ya MGR, na Kongani ya Viwanda ya Kwala – mradi mkubwa uliogharimu takribani trilioni 6.
Katika kongani hiyo, Rais Samia atazindua viwanda saba vilivyokamilika na kuanza uzalishaji pamoja na kutembelea viwanda vingine vitano vilivyopo katika hatua mbalimbali za ujenzi.