
05/09/2025
Mwimbaji wa nyimbo za injili kutoka Rwanda, Gloriose Musabyimana, anayejulikana zaidi kwa jina la Gogo, amefariki dunia nchini Uganda akiwa na umri wa miaka 36 baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kwa mujibu wa ripoti ya kitabibu kutoka Kyegera Doctors Center jijini Kampala, Gogo alifariki usiku wa Septemba 3, 2025. Taarifa hiyo imethibitishwa pia na Bikem Uwayesu, rafiki na mwakilishi wake wa karibu aliyekuwa naye katika ziara hiyo.
Uwayesu alisema Gogo alisafiri kutoka Rwanda tarehe 28 Agosti kuelekea Mbarara, Uganda, kuhudhuria mkutano wa injili uliofanyika kuanzia Agosti 29 hadi 31. Baada ya hapo, alielekea jijini Kampala kuendelea na shughuli za matangazo ya kazi zake za muziki.
Hata hivyo, mara baada ya kuwasili Kampala, alipatwa na maradhi. Awali walidhani ni hali ya kawaida kwani aliwahi kukumbwa na tatizo hilo kabla, lakini ghafla afya yake ilizorota.
Alikimbizwa hospitalini lakini alifariki dunia mara tu alipofikishwa.
Gogo alijulikana kupitia nyimbo zake za injili zilizovuma mitandaoni, hususan wimbo wake Blood of Jesus. Wimbo huo ulipata umaarufu wa kimataifa baada ya msanii kutoka Afrika Kusini, David Scott maarufu k**a The Kiffness, kuufanyia remix na kuuongeza ala za muziki wa tarumbeta na piano, kisha kuusambaza kupitia TikTok na YouTube mnamo Januari 2025.
Remix hiyo tayari imeangaliwa zaidi ya mara 780,000 kwenye YouTube.
Gogo aliwavutia wapenzi wengi wa muziki wa injili ndani na nje ya Rwanda. Kifo chake kimeacha simanzi kubwa katika tasnia ya muziki wa injili Afrika Mashariki, huku wapenzi na wadau wa muziki wakimtaja k**a upotevu mkubwa kwa kanisa na jamii ya muziki wa injili.