19/04/2025
BASHUNGWA AFUNGUA LIGI YA DK. SAMIA & KYOMBO - MISSENYI
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Innocent Bashungwa (Mb), amezindua Mashindano ya Mpira wa Miguu ya Dk. Samia & Kyombo Cup 2025 katika Uwanja wa Mashujaa, Bunazi, wilayani Missenyi, mkoani Kagera, leo tarehe 19 Aprili 2025.
Mashindano hayo yameandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Missenyi, Dkt. Florent Laurent Kyombo, na yanatarajiwa kushirikisha timu 20 kutoka kila kata ya wilaya hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Bashungwa amesema kuwa mashindano hayo yatasaidia kuibua vipaji vya michezo kwa vijana, kuimarisha afya, kuendeleza mshikamano na kudumisha upendo miongoni mwa vijana na wakazi wa Wilaya ya Missenyi.
“Mhe. Mbunge kwa kushirikiana na Madiwani wameonyesha dhamira ya dhati katika maendeleo ya michezo ndani ya Wilaya ya Missenyi. Ligi hii siyo tu burudani bali pia ni fursa kwa vipaji chipukizi. Naomba vijana kutoka kata zote 20 mshiriki kwa moyo wa upendo na mshikamano,” alisema Mhe. Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa ametoa wito kwa waamuzi na wasimamizi wa mashindano hayo kuhakikisha wanatenda haki wakati wa michezo yote, ili ligi hiyo imalizike kwa amani na kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Missenyi, Dkt. Florent Kyombo, amesema kuwa mashindano hayo yanalenga kuimarisha mahusiano na mshikamano kati ya vijana na wananchi wa kata zote 20 za wilaya hiyo.
Katika hafla ya uzinduzi, ambayo ilizikutanisha timu za kata za Kyaka na Mtukula, timu zote shiriki zilipatiwa vifaa mbalimbali vya michezo, ikiwemo jezi, mipira, vifaa vya mazoezi, pamoja na fedha kwa ajili ya maandalizi ya mechi.