
09/08/2025
Nyota wa tenisi kutoka Japani, Naomi Osaka, ameamua kujiondoa katika mashindano ya WTA 1000 ya Cincinnati ili kupata muda wa kupumzika na kujiandaa kikamilifu kuelekea US Open inayotarajiwa kuanza Agosti 24.
Uamuzi huo unakuja siku chache baada ya Osaka kushindwa kunyakuwa taji la pili mfululizo, akipoteza fainali ya Montreal dhidi ya bingwa chipukizi kutoka Canada, Victoria Mboko. Wakati wawili hao wakipambana kwenye fainali ya Montreal, mashindano ya Cincinnati tayari yalikuwa yameanza. Kwa mujibu wa ratiba, washindi wa Montreal walikuwa wamepewa nafasi ya kuingia moja kwa moja kwenye raundi ya pili ya Cincinnati.
Hata hivyo, Mboko alitangaza kujiondoa mara baada ya kushinda Canadian Open, wakati Osaka naye alisubiri kwa muda kabla ya kutoa uamuzi huo. Osaka alikuwa amepangwa kumenyana na Linda Noskova, huku Mboko akitarajiwa kumenyana na Diana Shnaider.