17/01/2026
WADAU WAOMBA ELIMU TOZO ZA HAKIMILIKI IONGEZWE, COSOTA WAFAFANUA
Wadau wa sanaa wakiwemo Sanaa za ufundi na kazi za maandishi, wachoraji na wachonga vinyago wameiomba serikali kuwapa kipaumbele katika fursa mbalimbali zinazowahusu, ikiwemo kushirikishwa katika makongamano mbalimbali na kupewa elimu ya mambo kadhaa yanayoweza kuwanufaisha ikiwemo elimu ya mirabaha.
Wadau hao wametoa maombi hayo ikiwa ni Siku chache baada ya serikali kuridhia kuanza kwa utekelezaji wa tozo mpya ya hakimiliki nchini, ambapo Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) inajiandaa kugawa mrahaba wa kwanza, unaotokana na tozo ya asilimia 1.5 ya thamani ya vifaa vinavyotumika katika kuzalisha, kuhifadhi na kusambaza kazi za sanaa na kazi za maandishi nchini, inayotozwa wakati wa uingizwaji au uzalishaji wa vifaa hivyo ambavyi ni pamoja na DVD, Recorder, Radio zinazorekodi na Televisheni zinazorekodi.
Akizungumza kuhusu Tozo hizo za Hakimiliki, Afisa wa Hakimiliki kutoka Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Judith Komba, amesema kwa mujibu wa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, fedha hizo takribani bilioni 1 zilizokusanywa, zinazotarajiwa kugawiwa kwa makundi hayo, zinatajwa kuwa zitawanufaisha wabunifu wa makundi yote, Kuanzia muziki, filamu, Sanaa za ufundi na kazi za maandishi, ambapo Hatua hii inatajwa kuwa mkombozi wa kiuchumi kwa wasanii, k**a ambavyo anafafanua Afisa wa Hakimiliki kutoka Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) Judith Komba.
Amesema kuwa licha ya kuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuanza kutoza tozo hiyo ya hakimiliki, si jambo geni kwa baadhi ya nchi nyingine za Afrika ambapo Kenya, Malawi, Morocco naTunisia ni baadhi ya nchi ambazo zimekuwa zikitoza tozo hizo.