SPARK LIGHT TV

SPARK LIGHT  TV Kwa Habari zote kali za Ndani na Nje ya Nchi,Uchumi ,Biashara ,Burudani na Michezo

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza mpango wa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi katika siku za karibuni, huku uk...
28/09/2025

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza mpango wa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi katika siku za karibuni, huku ukiwashukuru viongozi wa serikali kwa kuwezesha mazingira rafiki ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Afisa Habari wa TBA, Adam Mwingira, alisema hatua hiyo imechochewa na mabadiliko ya kisheria yaliyofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Sheria ya Majengo GN Namba 595 ya mwaka 2023. Marekebisho hayo yanaruhusu TBA kushirikiana na sekta binafsi pamoja na taasisi za kifedha ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ubora na kwa wakati.

Mwingira alisema kupitia fursa hiyo, TBA inawakaribisha wawekezaji wenye nia ya kushirikiana kwa njia ya ubia ili kuongeza ufanisi na kasi ya ujenzi wa miradi ya kimkakati nchini. Alisisitiza kuwa ushirikiano wa aina hiyo utasaidia kuongeza thamani ya miradi na kuleta manufaa kwa jamii kwa ujumla.

Aidha, aliainisha baadhi ya miradi mikubwa ambayo tayari TBA imeitekeleza, ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato na Hospitali ya Mkoa wa Geita, ambazo zimekuwa kichocheo cha kusogeza huduma za afya karibu zaidi na wananchi.

Aliongeza kuwa miradi hiyo imechangia kupunguza changamoto za upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wananchi wa maeneo hayo na kuongeza ustawi wa jamii kwa ujumla.

Mwingira pia alitaja kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, akibainisha kuwa ni moja ya vielelezo vya utekelezaji wenye tija unaofanywa na TBA katika kuboresha miundombinu ya umma.

Vilevile, alisema taasisi hiyo inatekeleza miradi mingine ikiwemo ujenzi wa ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwa mujibu wa TBA, utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha taasisi za umma zinakuwa na mazingira bora ya kufanyia kazi.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wachimbaji wa madini, hususan wa dhahabu, kujiunga na mfumo rasmi wa kifedha kwa k...
28/09/2025

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wachimbaji wa madini, hususan wa dhahabu, kujiunga na mfumo rasmi wa kifedha kwa kuuza dhahabu zao moja kwa moja kwa Benki Kuu ili kusaidia kukuza akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa taifa.

Meneja wa Uhusiano wa Umma na Itifaki wa BoT, Victoria Msina, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akimpa maelezo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, alipotembelea banda la BoT katika Maonesho ya Nane ya Madini yanayomalizika leo Septemba 28, 2025 mkoani Geita.

Msina alisema BoT imejikita katika kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati sambamba na kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi ya mifumo ya kifedha, ikiwemo uwekezaji katika dhamana za serikali kwa lengo la kuongeza ushirikiano kati ya sekta hiyo na taasisi za kifedha.

Aidha, alibainisha kuwa elimu hiyo inatolewa katika vituo mbalimbali vya BoT vilivyopo nchini pamoja na kupitia maonyesho na mikutano ya sekta ya madini, hatua inayolenga kuwakwamua wachimbaji kutoka kwenye mifumo isiyo rasmi.

Katika maonesho hayo, wachimbaji kutoka maeneo mbalimbali walijitokeza kutembelea banda la BoT ambapo walipata maelezo na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ya kifedha yanayohusu biashara ya madini.

“Tunawasihi waje tuwafundishe kwa sababu wakielewa mfumo huu, wataweza kujiinua kiuchumi na kuiwezesha serikali kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia uwekezaji wao kwenye dhamana,” alisema Msina.

Aliongeza kuwa BoT inatoa pia elimu ya fedha kwa wachimbaji juu ya namna bora ya kukopa kwa malengo, matumizi sahihi ya fedha na matumizi ya mifumo rasmi ya malipo inayosimamiwa na benki hiyo. “Unakopa kwa malengo, si kwa kununua vitu visivyo na maendeleo,” alisisitiza.

Benki Kuu ya Tanzania inatarajia kupitia ushirikiano huo wachimbaji wa madini watachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uchumi wa taifa pamoja na kujikwamua kiuchumi binafsi kupitia maarifa ya kifedha na uwekezaji rasmi.

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Ahmed Said, amepongeza jitihada za Benki Kuu ya Tanzania (Bo...
28/09/2025

Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Ahmed Said, amepongeza jitihada za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi kupitia banda lake katika Maonyesho ya Nane ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini Mkoani Geita. Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Zena alisema elimu hiyo ni muhimu kwa ustawi wa kiuchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla.

Katika banda hilo la BoT, wananchi walipata mafunzo ya namna bora ya kuwekeza fedha zao, hasa kwenye dhamana za Serikali, ambazo zimeelezwa kutoa faida kubwa na salama kwa wawekezaji. Katibu Mkuu Kiongozi alisema kuwa elimu hii itasaidia wananchi wenye fedha kutambua njia sahihi za kuzitumia kwa maendeleo yao na ya taifa.

“Kuna watu wana fedha zao nyingi lakini hawajui jinsi ya kuziwekeza. Kupitia elimu hii, sasa wanaweza kuelekezwa kuwekeza kwenye dhamana za Serikali ambazo ni salama na zenye tija,” alisema Zena.

Mbali na elimu ya uwekezaji, BoT pia inatoa mafunzo kuhusu namna ya kujiepusha na vitendo vya utakatishaji wa fedha, ambacho ni tatizo la kimataifa linaloweza kuiingiza nchi kwenye matatizo ya kifedha na kisheria. Zena alisema elimu hii itawasaidia wananchi kuelewa madhara ya kushiriki au kuhusishwa na vitendo hivyo haramu.

Aidha, alieleza kuwa masuala mengine ya kifedha yanayotolewa katika banda la BoT ni pamoja na mbinu za kusimamia fedha za kaya, kuweka akiba, na kuongeza maarifa ya kifedha kwa wajasiriamali wadogo na wa kati. Alisisitiza kuwa elimu hiyo inawawezesha wananchi kufanya maamuzi ya kifedha kwa ujasiri na ufanisi.

Zena aliongeza kuwa maonyesho hayo hayakubaki tu kwa wachimbaji na wadau wa sekta ya madini, bali pia yamewaunganisha wajasiriamali kutoka Tanzania Bara, Visiwani na hata nje ya mipaka ya nchi. Kwa mujibu wake, ushirikishwaji huo ni fursa ya kipekee ya kujenga mtandao mpana wa kibiashara na ushirikiano wa maendeleo.

27/09/2025

Zaidi ya mabinti 100 wanaosomea kozi za afya katika ngazi ya diploma wanatarajiwa kunufaika na fedha zitakazopatikana kupitia Shen Marathon, mbio maalum zinazolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kugharamia ada ya masomo kwa wanafunzi wa k**e waliokumbwa na changamoto za kifedha.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, mwanzilishi wa Shen Marathon, Elizabeth Ntungu, ambaye pia ni mwamuzi wa kandanda wa k**e, amesema kuwa lengo kuu la mbio hizo ni kuwasaidia mabinti wanaotaka kutimiza ndoto zao kupitia elimu, lakini wanakumbwa na vikwazo vya kifedha.

“Zaidi ya mabinti 100 watanufaika moja kwa moja na fedha zitakazopatikana kupitia marathon hii. Tunawahamasisha Watanzania kushiriki kwa wingi ili kwa pamoja tuwe sehemu ya mabadiliko ya maisha ya hawa watoto wa k**e,” alisema Elizabeth.

Marathon hiyo imepangwa kufanyika tarehe 25 Oktoba 2025, katika viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam, ikitarajiwa kuwashirikisha washiriki kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo wanamichezo, wasanii, wanafunzi, mashirika, na wananchi wa kawaida.

Kwa upande wake, Carry Mastory, mmoja wa waratibu wa tukio hilo, alisema kuwa ada ya ushiriki ni Shilingi 30,000 tu, na fedha zote zitakwenda moja kwa moja kusaidia kugharamia ada ya mabinti wanaosomea afya.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ametoa rai kwa Bodi ya Bima ya Amana kuendelea kupanua wigo wa huduma zake ili ku...
27/09/2025

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ametoa rai kwa Bodi ya Bima ya Amana kuendelea kupanua wigo wa huduma zake ili kuhakikisha mitaji ya Watanzania, hususan katika vikundi vidogo vya kifedha k**a SACCOS na VICOBA, inabaki salama. Akizungumza mjini Geita, Komba alisema Watanzania wengi bado wanawekeza fedha katika maeneo ambayo hayajasajiliwa rasmi, hali inayowaletea hasara kubwa pale vikundi hivyo vinapovunjika.

Komba alieleza kuwa katika ofisi za wakuu wa wilaya, mara kwa mara wananchi wamekuwa wakifika kulalamikia kupoteza akiba kubwa walizowekeza. “Unampokea mwananchi anakwambia amewekeza milioni 30 kwenye kikundi cha kifedha lakini zote zimepotea. Tunaanza kuhangaika kumtafuta kiongozi wa kikundi bila mafanikio. Ni wakati sasa wa kuongeza kasi ya kuhakikisha mitaji ya Watanzania inalindwa,” alisema.

Ameongeza kuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inapaswa kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Bima ya Amana kushuka chini kwa kasi kubwa ili kufikia taasisi ndogo ndogo.

Kwa upande wake, Mkuu wa kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa Bodi ya Bima ya Amana, Lwaga Mwambande, amesema Kwa niaba ya DIB amepokea ushauri wa Mkuu wa Wilaya ya Geita na kusisitiza kuwa ushirikiano na wadau wengine wa sekta ya fedha utaendelea kuimarishwa kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanakuwa na imani katika mfumo rasmi wa kifedha nchini.

Mwambande alifafanua kuwa kwa sasa kinga inayotolewa na bodi hiyo ni Shilingi milioni 7.5 kwa kila mteja endapo benki itafungwa. “Kinga hii inawafikia wananchi wengi kwani asilimia 99 ya wenye amana wanalindwa. Hii inatupa nafasi ya kuendelea kuwahakikishia Watanzania usalama wa fedha zao katika taasisi za kifedha zilizosajiliwa,” alieleza.

Hata hivyo, Mwambande alikiri kuwa bado ipo haja ya kuangalia namna bora ya kufikia vikundi vya kifedha visivyo rasmi, k**a vile VICOBA na SACCOS, ili kuhakikisha Watanzania wanaotumia mifumo hiyo pia wananufaika na ulinzi wa mitaji yao.

Ameongeza kuwa pamoja na jukumu la kuwalipa fidia wananchi endapo benki ikifungwa, lengo kubwa la Bodi ya Bima ya Amana ni kujenga imani ya kudumu kwa wananchi kuhusu mfumo wa kifedha.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa jitihada zake za kuendelea kutoa elim...
26/09/2025

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa jitihada zake za kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya kifedha kupitia maonyesho ya madini yanayoendelea mkoani humo. Amesema elimu hiyo imekuwa chachu kubwa ya kuelimisha wananchi juu ya namna bora ya kutumia taasisi za kifedha zilizosajiliwa, hasa katika kipindi ambacho changamoto ya mikopo isiyo rasmi imekuwa ikiwakumba wananchi wengi.

Katika ziara yake kwenye mabanda ya maonyesho hayo, Komba alitembelea kitengo cha usimamizi wa masuala ya fedha, usimamizi wa benki na mikopo. Amebainisha kuwa, kwa muda mrefu wananchi wa maeneo mbalimbali wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya taasisi zisizosajiliwa ambazo hutoa mikopo kwa riba kubwa na hatimaye kuwaumiza wateja wao.

“BoT ina kitengo maalum kinachohakikisha taasisi zinazotoa mikopo kwa wananchi zimesajiliwa na zinafuata sera za kifedha za Taifa. Hii ni hatua muhimu ya kulinda wananchi dhidi ya taasisi zinazokopesha bila kufuata sheria na kuwafilisi wananchi wetu,” alisema Komba.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kufurahishwa kwake na hatua ambazo serikali imekuwa ikichukua mara baada ya kupokea taarifa za taasisi zinazowakopesha wananchi bila usajili. Alisema baadhi ya wananchi, akiwemo wajane, wamepoteza mali zao ikiwemo nyumba baada ya kushindwa kurejesha mikopo ya riba kubwa, lakini uchunguzi umebaini taasisi hizo hazikuwa zimesajiliwa.

Kwa mujibu wake, wananchi wanapaswa kuacha kukimbilia mikopo rahisi kutoka kwa taasisi zisizotambulika, bali wajenge utamaduni wa kutumia taasisi zinazotambuliwa na BoT. Amesema njia hiyo itarahisisha mamlaka kuchukua hatua pale changamoto zinapotokea, na hivyo kuwalinda watumiaji wa huduma hizo.

Katika ziara hiyo, Komba pia alishuhudia ushirikiano wa karibu kati ya BoT na Bodi ya Bima ya Amana (DIB), ambao unalenga kulinda mali na amana za wananchi walioweka fedha zao katika taasisi za kifedha zilizosajiliwa. “Hii ni faida kubwa kwa wananchi kwani hata taasisi ikipata changamoto, bado kuna chombo cha kisheria kinachowalinda,” alisisitiza.

Tafiti zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 70 ya ubunifu mpya wa teknolojia duniani unahusishwa moja kwa moja na taaluma ...
25/09/2025

Tafiti zinaonesha kuwa, zaidi ya asilimia 70 ya ubunifu mpya wa teknolojia duniani unahusishwa moja kwa moja na taaluma ya uhandisi ambayo ndani yake hujumuisha masuala mbalimbali ikiwemo Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Nishati, viwanda na  akili mnemba. 

Hayo yamebainishwa Septemba 25, 2025 jijini Dar es Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kufungua Maadhimisho ya 22 ya Siku ya Waandisi kwa Mwaka 2025.

Amesema kuwa Serikali inawahitaji na kuwategemea wahandisi nchini ambao wana fursa ya kuchangia maendeleo ya nchi kupitia utekekezaji wa majukumu yao.
Dkt. Biteko ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya uvumbuzi na maendeleo ya viwanda huhitaji huduma ya wahandisi moja kwa moja.

“ Kwa niaba ya Serikali naomba niwakumbushe kuwa taifa linawategemea sana. Tunawategemea, tunawahitaji naomba mjue Serikali itaendelea kuwategemea wakati wote mnapotekeleza majukumu yenu,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko ameitaka ERB kuwasaidia wahandisi nchini kwa kuwaelekeza na kuwapa motisha pale wanapofanya vizuri badala ya kubaki kuwa tishio kwao na kuwapa adhabu baada ya kukosea.

Ameendelea kusema motisha  kwa wahandisi wazawa walioshiriki katika ujenzi wa miradi ya kimkakati nchini sambamba na kuwapa hamasa na kuwajengea uwezo wa kushiriki miradi mingine ya kimkakati ni muhimu ili kuwapata wahandisi wazalendo

Naye, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa Wizara itaendelea kuimarisha mazingira ya taaluma ya uhandisi ikiwa ni pamoja na kuruhusu mafunzo ya kuongeza viwango vya taaluma hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Menye Manga amesema katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imetekeleza miradi mikubwa ikiwemo



25/09/2025

Mkurugenzi Mtendaji wa Mafyaa Boxing Center, Ally Zayumba, amezindua rasmi msimu wa sita wa Knockout ya Mama, tukio maarufu la ngumi linalolenga kukuza na kuendeleza vipaji vya mabondia nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Zayumba alieleza kuwa msimu huu utafuatiwa na tamasha kubwa la ngumi, litakalofanyika jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Kijitonyama, mnamo tarehe 10 Oktoba.

"Lengo letu ni kuonyesha maendeleo ya mchezo wa ngumi hapa nchini, sambamba na kutoa burudani ya hali ya juu kwa mashabiki wa ngumi," alisema Zayumba. Aidha, alibainisha kuwa maandalizi ya tamasha hilo yanaendelea vizuri na akaongeza wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kuunga mkono na kushuhudia vipaji vya mabondia wa ndani.

Tamasha hili linatarajiwa kuwa kivutio kikubwa katika kalenda ya michezo, likiwa ni jukwaa la kukuza vipaji, kuhamasisha ushiriki wa vijana, na kuimarisha mchezo wa ngumi Tanzania.

Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, John Faustine, ameupongeza uanzishwaji wa maon...
25/09/2025

Meneja wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, John Faustine, ameupongeza uanzishwaji wa maonyesho ya madini yanayofanyika katika mkoa huu, akisema ni fursa muhimu kwa wadau wa sekta ya madini kujifunza na kupata mwongozo wa kitaalamu juu ya matumizi salama ya kemikali.

Akizungumza kwenye maonyesho hayo, Faustine alisema kuwa mamlaka hiyo ipo kwa lengo la kuhakikisha wadau wanaojishughulisha na madini na kemikali wanafuata sheria na kanuni zinazohusiana na usalama wa binadamu na mazingira. “Mkemia Mkuu wa Serikali ana jukumu la usajili wa kemikali zote nchini, kutoa vibali vya kuingiza na kusafirisha kemikali, pamoja na kusajili wadau na maeneo wanayoyatumia kemikali,” Faustine alisema.

Faustine alisema kuwa mamlaka inatekeleza majukumu mawili makuu: usimamizi wa sheria za kemikali na uchunguzi wa kimaabara wa ubora na usalama wa kemikali. “Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali Majumbani, ya mwaka 2003, ni muhimu sana kwa sababu shughuli nyingi za binadamu zinahusisha kemikali. Kwa hivyo, ni lazima kuwe na miongozo inayotekeleza matakwa ya sheria hizi,” alisema.

Aliongeza kuwa katika uchenjuaji wa madini k**a dhahabu, ni muhimu kwa wachimbaji kuelewa kiwango cha dhahabu kilichopo kwenye udongo na madini yanayoweza kushindana na kemikali zinazotumika. “Kemikali hizi zina tabia ya ‘kutafuna’ madini pale zinapokuwa zikitumika. Hivyo, wachimbaji wanashauriwa kupeleka udongo wao kwenye maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kabla ya kuanza uchenjuaji ili kubaini kiasi cha dhahabu na madini jirani k**a silva, kopa, na salfa, ili uchenjuaji uwe rahisi na salama,” Faustine alisema.

Mamlaka hiyo pia imewatoa wito wadau wote wa kemikali kuhakikisha wanatumia kemikali kwa taratibu salama. Faustine alisisitiza kuwa matumizi mabaya ya kemikali yanaweza kuathiri afya ya binadamu, jamii na mazingira. “Kemikali ikishaingia ardhini haina mpaka. Hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha mazingira yetu na jamii ziko salama,” alisema.

Maonyesho hayo yamekuwa pia ni jukwaa la wadau kujifunza na kutatuliwa changamoto zao na wataalamu wa mamlaka, huku ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ikitoa mwongozo wa kitaalamu kwa wachenjuaji na wadau wengine wanao

Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) tawi la Geita umeshiriki katika Maonesho ya Nane ya Kimataifa ya Madin...
25/09/2025

Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) tawi la Geita umeshiriki katika Maonesho ya Nane ya Kimataifa ya Madini kwa lengo la kuelimisha umma juu ya kazi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kusimamia mtandao wa barabara za wilaya.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TARURA Geita, David Msechu, alisema kuwa taasisi hiyo inahakikisha ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara za wilaya ili kusaidia ukuaji wa uchumi na huduma za jamii. “Kwa sasa, TARURA inasimamia mtandao wa barabara wa kilomita 100,044 nchini kote, huku mkoa wa Geita ukihudumiwa na mtandao wenye urefu wa kilomita 7,264, ambao unapitika kwa asilimia 60,” alisema Msechu.

Aliongeza kuwa kati ya mtandao huo, kilomita 564 ni barabara zinazohudumia maeneo ya madini. “Tunaendelea kushirikiana na wadau wa madini kuhakikisha barabara hizi zinaboresha upatikanaji wa malighafi na huduma za kijamii, huku tukitenga fedha maalum kwa ajili ya miradi ya matengenezo,” alisema.

Kwa mujibu wa Msechu, kwa mwaka wa fedha 2024/25 na 2025/26, TARURA imetenga shilingi milioni 580 kwa ajili ya kukamilisha kilomita 210 za barabara zinazohudumia maeneo ya madini, huku baadhi ya kazi zikiwa zimekamilika na zingine zikiendelea. Sambamba na hilo, TARURA Geita ina maabara ya kisasa ya kupima ubora wa barabara, ambayo inahudumia miradi mbalimbali ya ujenzi, umwagiliaji, miradi ya TANESCO, na miradi ya Ruwasa.

“Tuna miradi ya lami yenye urefu wa kilomita 17, ujenzi wa stendi, na madaraja kadhaa, yote yakitumia teknolojia ya kisasa kuhakikisha ubora,” alisema Msechu. Aliwataka wananchi na wadau wa madini kushirikiana ili kuepuka kuharibika kwa barabara kutokana na mizigo mizito isiyozidi viwango vinavyoruhusiwa.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Miradi TARURA kutoka Makao Makuu, Faiza Mbande, alisema kuwa taasisi hiyo pia inatoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya barabara. “Tunawaelimisha wananchi kuepuka kupitisha wanyama barabarani, kulima pembezoni mwa barabara, na usafirishaji wa mizigo mizito, pamoja na kuwashirikisha kuhusu masuala ya fidia,” alisema Mbande.

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum (TISEZA) imetangaza rasmi fursa za uwekezaji katika sekta ya madini kupitia eneo m...
25/09/2025

Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum (TISEZA) imetangaza rasmi fursa za uwekezaji katika sekta ya madini kupitia eneo maalum la Buzwagi lililoko Kanda ya Ziwa. Ofisa Uwekezaji Mkuu wa Kanda hiyo, Erastus Malai, amesema eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 1,333 limetengwa mahsusi kwa ajili ya shughuli za uchenjuaji madini.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza fursa hizo, Malai alisema eneo la Buzwagi limeandaliwa kwa kuzingatia mahitaji ya wawekezaji ili kuhakikisha mchakato wa kuwekeza unakuwa rahisi na wa haraka. "Tumeweka miundombinu yote muhimu, kuanzia barabara, majengo, ofisi hadi uwanja wa ndege. Mwekezaji akifika hatalazimika kugharamia miundombinu, isipokuwa kuwekeza moja kwa moja kwenye kiwanda cha uchenjuaji madini," alisema.

Mbali na Buzwagi, TISEZA pia imetenga maeneo mengine maalum nchini kwa ajili ya uwekezaji katika sekta mbalimbali. Malai alitaja maeneo hayo kuwa ni Nara mkoani Dodoma lenye ekari 607, Wara Kibaha mkoani Pwani lenye ekari 100 na Bagamoyo lenye ekari 151. "Maeneo haya yametengwa kwa uwekezaji kwenye viwanda vya dawa na vifaa tiba, magari na boti, bidhaa za ngozi, nguo, makazi na vifaa vya majumbani," aliongeza.

Aidha, Malai alibainisha kuwa uzinduzi wa maeneo hayo ni hatua mpya kwa mamlaka hiyo katika kukuza sekta ya uwekezaji nchini. Alisema mpango huo unalenga si tu kuendeleza sekta ya madini, bali pia kutoa fursa za kiuchumi kwenye nyanja nyingine muhimu.

Kwa mujibu wa Malai, fursa nyingine zilizoko Kanda ya Ziwa ni pamoja na uwekezaji katika sekta za kilimo, uvuvi, utalii, ujenzi wa majengo ya biashara na ufugaji. "Tunaamini maeneo haya yatakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi wa taifa na ajira kwa wananchi," alisema.

TISEZA imesisitiza kuwa serikali ipo tayari kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kodi kwa wawekezaji watakaowekeza kwenye maeneo hayo, hususan eneo maalum la Buzwagi. Vivutio hivyo vinatarajiwa kuongeza mvuto wa uwekezaji na kuhakikisha mwekezaji anapata unafuu wa gharama.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, ameipongeza Taasisi ya Nyumba Tanzania (TBA) kwa kuja na wazo la kuanzis...
25/09/2025

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Grace Kingalame, ameipongeza Taasisi ya Nyumba Tanzania (TBA) kwa kuja na wazo la kuanzisha mradi mkubwa wa Makazi ya Biashara mkoani Geita, akisema mradi huo ni kielelezo cha tafsiri ya maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora.

Akizungumza Septemba 24, 2025, alipotembelea maonyesho ya nane ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, Kingalame alisema uamuzi huo wa TBA ni hatua muhimu ya kuimarisha ustawi wa wananchi kupitia miradi ya kimkakati ya makazi.

“Nimekuja kushuhudia wazo hili la kuanzisha mradi mkubwa wa Makazi ya Biashara mkoani Geita. Hii ni tafsiri ya maono ya Rais Dkt. Samia, anatamani watu wake wakae kwenye maeneo mazuri na yenye hadhi,” alisema Kingalame.

Aidha, alitoa pongezi kwa TBA kwa uamuzi wa kukaribisha sekta binafsi kushirikiana nao, akisema ushirikiano huo utasaidia kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.

“Naomba sekta binafsi ichangamke kushirikiana na TBA ili makazi haya yakamilike kwa muda muafaka. Hii italeta raha kwa sababu watumishi na wananchi kwa ujumla watapata makazi bora ya kuishi,” alisisitiza.

Mradi huo wa Makazi ya Biashara mkoani Geita unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, huku ukitarajiwa kuongeza thamani ya mji wa Geita na kutoa suluhisho la changamoto za makazi kwa wananchi na watumishi wa umma.

Address

Dar Es Salaam
Dar Es Salaam
45180

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when SPARK LIGHT TV posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Business

Send a message to SPARK LIGHT TV:

Share