
18/07/2025
Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, limepinga agizo la serikali, kuwataka wasichana waliopata mimba kuendelea na masomo. Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki CENCO, limesema Shule zake hazitatekeleza agizo hilo la serikali.
Kupitia barua ya wazi, walioijibu serikali kupitia Wizara ya Elimu, Kanisa Katoliki ambalo lina Shule zaidi ya 18, 000 linasema, agizo hilo la serikali linakwenda kinyume na kanuni za kupata elimu nchini humo.
Aidha, Kanisa hilo linasema kuwaruhusu wasichana waliopata mimba kuendelea na masomo, wakiwa wajawazito, kutasababisha upotofu mkubwa wa maadili na nidhamu miongoni mwa wanafunzi.
Kanisa hilo linasisitiza kuwa halitakuwa tayari, kuwa na msichana mjazito darasani, na badala yake, watakaokuwa katika hali hiyo, watahamishiwa kwenye shule za serikali.
Mvutano huu unakuja wakati huu Katiba ya DRC, ikitoa usawa wa watu wote kupata elimu lakini kwa muda mrefu wasichana wajawazito wamekuwa wakitengwa na kuacha masomo.