22/11/2022
Isaya 35:1-10
[1]Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua k**a waridi.
[2]Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa BWANA, ukuu wa Mungu wetu.
[3]Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.
[4]Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.
[5]Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.
[6]Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka k**a kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.
[7]Na mchanga ung’aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi.
[8]Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.
[9]Hapo hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapanda juu yake; hawataonekana hapo; bali waliokombolewa watakwenda katika njia hiyo.
[10]Na hao waliokombolewa na BWANA watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia.