12/12/2025
Waziri wa Maji, Juma Awesu amesema, tatizo la maji Dar es Salaam limesababishwa na kutokuwepo mvua za kutosha hivyo kuathiri uzalishaji wa maji.
Akizungumza kwa simu kwenye kikao cha Wahariri na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (DAWASA), Waziri Awesu ameagiza DAWASA kuweka wazi ratiba ya ugawaji maji ili kuepuka upendeleo na malalamiko.
“Sasa hivi kuna ukamwe, mvua zimechelewa kunyesha na hili sio jambo la kuficha, niwaombe radhi Wananchi wa Dar es Salaam kutokana na upungufu huo. Niwaombe tuwe wavumilivu katika kipindi huki cha mpito.
" Nimeagiza kiwango hiki kidogo cha uzalishaji kwa sasa, DAWASA waweka wazi na usawa ratiba ya ugawaji maji ili kuepuka malalamiko,” amesema Awesu.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mk**a Bwire amesema, mtambo uliothirika zaidi ni Ruvu Chini ambapo sasa unazalisha lita 50,000,000 badala ya lita 270,000,00 kwa siku.
Amesema, hatua za haraka zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kurejesha maji ya Mto Ruvu yaliyokuwa yakipotea kwenye njia yake, kufufua visima virefu na kuchimba visima vipya, kusimamisha vibali vya matumizi mengine ya maji na kudhibiti mivujo ya maji.
Amesema, katika utatuzi wa kudumu wa tatizo la maji Dar es Salaam, tayari Serikali ya Awamu ya Sita inajenga Bwawa la Kidunda ambapo linatarajiwa kukamilika Disemba 2026.
“Lengo la Bwawa la Kidunda ni kuhifadhi maji ambapo yataweza kutumika katika kipindi k**a hiki. Tsh. 336 Bilioni zinatumika kuhakikisha bwawa hili linakamilika na mpaka sasa limefika asilimia 35 ya ujenzi wake,’ amesema Bwire.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameshauri kuwepo kwa taarifa za mara kwa mara kwa wananchi kuhusu huduma za maji ili wawe kwenye mazingira mazuri ya kujipanga.