31/07/2025
Bunge la Rwanda limepitisha kwa kauli moja makubaliano ya amani kati yake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Makubaliano hayo yalisainiwa Juni 27, 2025 mjini Washington chini ya usimamizi wa Marekani, na kupitishwa rasmi na Bunge Julai 30 jijini Kigali.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, aliwaeleza wabunge kuwa Rwanda haitalegeza hatua zake za kiusalama hadi kundi la waasi la FDLR litakapoangamizwa. Pia alisisitiza umuhimu wa Kinshasa kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo k**a ishara ya dhamira ya kweli ya kurejesha amani ya kudumu.
Baada ya kupitishwa na Bunge la Rwanda, mkataba huo sasa utapelekwa kwenye Seneti kwa hatua zaidi. Kwa upande wa DRC, bado hakuna taarifa rasmi ya kuwasilishwa kwa mkataba huo bungeni, kwani Bunge lao liko likizoni, japo baadhi ya wabunge wameomba suala hilo lijadiliwe mara moja likirejea.
Katika kuendeleza utekelezaji wa makubaliano hayo, Rwanda na DRC zinatarajiwa kukutana wiki hii mjini Washington kwa kikao cha kwanza cha Kamati ya Pamoja ya Kusimamia Makubaliano. Kamati hiyo itaangazia malalamiko, uchunguzi wa ukiukwaji, utatuzi wa migogoro, na mapendekezo ya hatua stahiki kuhakikisha amani ya kweli inafikiwa.