28/08/2026
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, amesema uteuzi wa Deogratius Ndejembi kuwa Makamu wa Rais umetimiza ujumbe wa kiimani aliomweleza Ndejembi takribani miezi miwili iliyopita.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo, Ijumaa, Agosti 28, 2026, Kingu amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Ndejembi, akisema hatua hiyo imeonesha namna Rais anavyowaamini na kuwathamini vijana katika uongozi wa Taifa.
Kingu amesema uteuzi huo ni kutambua na kuthamini vijana waliolelewa katika misingi ya unyenyekevu, uadilifu, uzalendo, uchaji Mungu na kulipenda Taifa.
“Nchi yetu inapata kijana mwenye kaliba ya kuwapenda watu, mnyenyekevu, anayejishusha na mkarimu,” amesema Kingu.
Amesema Ndejembi amedhihirisha uzalendo katika utekelezaji wa majukumu yake, akitoa mfano wa namna alivyoshiriki katika kuhakikisha Taifa linapata uhakika wa upatikanaji wa mafuta kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wakati dunia ilipokuwa ikikabiliwa na misukosuko ya gharama na upatikanaji wa mafuta.
Akizungumzia kile kinachoelezwa kuwa ni unabii kuhusu uteuzi huo, Kingu amesema miezi miwili iliyopita alimtafuta Ndejembi kwa simu na kumweleza kuwa alikuwa amefunuliwa kuhusu jambo kubwa ambalo Mungu angeenda kumfanyia.
“Miezi miwili iliyopita Mungu alizungumza na mimi. Nilimpigia simu Ndejembi na kumtumia message kwamba nimefunuliwa na Mungu kwamba kuna jambo Mungu anakwenda kukufanyia,” amesema Kingu.
Ameongeza kuwa alimweleza Ndejembi: “Mungu amezungumza na mimi, nimekuona unapanda kwenye red carpet.”
Kingu amemtaka Ndejembi kutumia nafasi hiyo kumsaidia Rais Samia, akisema anapaswa kuhakikisha Rais anapata utulivu na matumaini katika kutekeleza ahadi zilizotolewa kupitia Ilani ya Uchaguzi.
“Nenda kamsaidie Rais, kamfanye Rais wetu apate utulivu, awe na matumaini makubwa ya kutekeleza ahadi tulizozitoa kupitia Ilani,” amesema.
Kingu ameahidi kuwa wabunge wataendelea kuwa wanyenyekevu na kutoa ushirikiano kwa Rais Samia, Makamu wa Rais Ndejembi na Waziri Mkuu katika kuliongoza Taifa.