17/09/2025
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ikiwa atachaguliwa na Watanzania katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, ameahidi kuendelea kulinda amani, uhuru, umoja na utulivu nchini k**a sehemu muhimu za kulinda na kuenzi kazi kubwa iliyofanywa na waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Sheikh Amani Abeid Karume.
Dkt. Samia ameyaeleza hayo leo Jumatano Septemba 17, 2025, siku ya kwanza ya kampeni zake Visiwani Zanzibar kwenye Kijiji cha Kajengwa, Makunduchi, akiahidi pia kuulinda muungano na mafungamano yaliyopo Kati ya Tanzania bara na Tanzania Zanzibar.
“Naweza kusema Muungano wetu sasa umekuwa Muungano wa udugu wa damu zaidi kuliko vigezo vingine vyote. Pamoja na Muungano wetu tumeweza pia kulinda Uhuru na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na hali kadhalika kudumisha umoja, amani na utulivu nchini. Hizi ndizo tunu kuu na za msingi kwa maendeleo ya nchi yetu na hizi niwaambie tutazilinda kwa bidii zetu zote.” Amesisitiza Dkt. Samia.
Dkt. Samia amesema tunu hizo muhimu za Taifa zimeijengea Tanzania utambulisho wa pekee Kikanda na Kimataifa pamoja na kukuza mahusiano ya Kidiplomasia duniani, suala ambalo limeifanya Tanzania kuwa Mbia muhimu na wa kutegemewa Kikanda na Kimataifa pamoja na kufungua milango ya ushirikiano na fursa zaidi kwa watanzania Kimataifa
Aidha katika hatua nyingine ya kuonesha uthabiti katika kusimamia tunu hizo, Dkt. Samia ambaye ni mwanamke wa kwanza kupitishwa katika Historia ya CCM kuwania nafasi hiyo, ameahidi kuanzisha Kituo cha kumbukumbu na nyaraka za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, k**a sehemu ya kuhifadhi urithi wa Muungano na kujenga uelewa wa pamoja kwa watu kujifunza zaidi kuhusu Muungano na sababu za uwepo wake.