24/03/2025
Harakati za utafutaji zikiwa zinaendelea ili kutafuta chochote kitu, simu inaita kutoka kijiweni huko wajumbe wanasema kuna barua imetumwa inahitajika kusomwa kila mwanakijiwe asikie kilichoandikwa. K**a mwanakijiwe mtiifu wito nikaitikia kufahamu yaliyomo ndani ya barua ngeni kutoka kusikojulikana.
Sio barua ya mapenzi wala barua ya urafiki hii ni barua kwenda kwa mtu aliyeamua kuziba masikio na kuinua macho yake kutizama mbele lengo ni kutengeneza historia yake na hakika vitabu vya kumbukumbu havitoliacha jina lake katika kurasa za mbele.
“Salamu kutoka ng’ambo ya mbali ziwafikie kwenu wanakijiwe wote, tupo ndani ya miezi mitakatifu (Ramadan & Quaresma) ni tumaini letu mnaendelea vizuri na kwa wenye matatizo M/mungu awape kheri, tumeona itakua ajabu tusipowatumia barua hii nanyi muisome kwa nguvu.
Ndugu wanakijiwe vitabu vya historia pale England havitolisahau jina la mfalme wa Egypt aliyeamua kwenda kusimika utawala wake mbali na nyumbani, huko katika ardhi ya kigeni na watawaliwa hawakuuchoka utawala wake.
Ndugu wanakijiwe katikati ya mazoea ya mchezaji yoyote bora hawezi kutoka nje ya nchi yao kutokana na malipo mazuri, mfalme huyu amezikacha pesa za visima vya mafuta na kutimkia ughaibuni na huko ndiko jina lako lilikokua limechorwa kabla ya ujio wake.
Ndugu wanakijiwe huenda ilikua ni kiwango kisichoridhisha kilichowafanya wababe wa pale kwao wasimfikirie tangu udogoni mwake lakini kwake yeye ilikua ni ahueni ya kuweza kutoka nje mikono ya wakubwa hao ambao wanaamini yoyote bora lazima awe kwao.
Ndugu wanakijiwe Mo Salah amezunguuka sana lakini Liverpool iliandikwa kwa ajili yake na ameitendea haki nafasi yake, kwa misimu yote aliyokuwepo amekua na muendelezo mzuri namba zake hazijawahi kuchuja, mpaka sasa amekua sehemu ya wafungaji bora wa muda wote wa ligi ya England akiwa ni mfalme kutoka Afrika katika nchi ya Egypt, nchi ambayo hapo mwanzoni waliamini haina haja ya kucheza nje ya kwao kwasababu ya pesa nono wanayoipata nyumbani.”
Ndugu wanakijiwe tulitamani kuandika mengi lakini barua yetu imeishia hapo na kwa hayo machache tuseme Wasalaam!.