
29/09/2025
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umekemea vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kuwazuia waumini wao kushiriki kwenye shughuli za kisiasa, wakieleza kuwa hatua hiyo inapingana na misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Mohamed Ali Kawaida, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Tanga, alisema amesikitishwa na kauli iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Septemba 25 mwaka huu huko Kipalapala, Tabora, kuhusu waumini kushirikiana na wanasiasa.
Kawaida alisema kauli hiyo imeonekana kwenye kipande cha video (klipu) kilichosambaa, ambapo kiongozi huyo alizungumzia masuala ya uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi. Aliongeza kuwa matamshi hayo ni kinyume na Katiba, kwani kila Mtanzania ana haki ya kushiriki katika shughuli za kisiasa bila kubaguliwa.