30/09/2025
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika ujenzi wa barabara muhimu wilayani Same ili kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo na kufungua fursa mpya za maendeleo.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 30, 2025, Dkt. Samia alisema kuwa ujenzi wa barabara ya Mkomazi–Kisiwani–Same yenye urefu wa kilomita 101 tayari umeanza na kugawanywa katika vipande viwili.
“Kipande cha kwanza ni Mkomazi–Ndungu chenye kilomita 36 ambapo ujenzi umeanza kwa gharama ya shilingi bilioni 59, na mkandarasi ameshakamilisha kilomita 10. Aidha, kipande cha pili cha Mroyo–Same chenye kilomita 65 mkandarasi amepatikana na tumeshasaini mkataba. Tunachosubiri sasa ni malipo ya awali ili kazi ianze mara moja,” alisema Dkt. Samia.
Aliongeza kuwa Serikali inatambua changamoto za usafirishaji wa zao la tangawizi linalolimwa kwa wingi katika tarafa za Mamba na maeneo mengine ya milimani, na hivyo imepanga kujenga barabara hizo kwa kiwango cha zege na lami ili kurahisisha usafirishaji wa mazao.
“Niwaahidi barabara hizi muhimu tutazikamilisha kwa viwango bora. Mungu akituwezesha, tutaendelea kufanya kazi hii ili kila mkulima anufaike,” alisisitiza.