
11/09/2025
TATHMINI YA MCHANGO WA WANAHABARI JUU KURIDHISHWA NA USAHIHI WA UTABIRI WA HALI YA HEWA
Dar es Salaam; Tarehe 10 Septemba, 2025
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini ili kujadili utabiri wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba ā Desemba) 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Usafirishaji (NIT). Akizungumza wakati wa mkutano huo Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Changāa alisema kupitia warsha hizi uelewa wa wanahabari kuhusu masuala ya hali ya hewa umeendelea kuimarishwa kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwezesha taarifa zitolewazo na mamlaka kufikia jamii kwa urahisi na kwa wakati.
āMnamo mwezi Julai mwaka 2025, Mamlaka iliandaa Dodoso maalumu kwa wanahabari ili kufanya tathmini ya utendaji kazi wake kwa Tasnia ya Habari, ambapo kwa taarifa niliyonayo ni kwamba tathmini hiyo imekamilika na matokeo yake yanaonesha asilimia 95 ya wanahabari waliotoa maoni yao wameridhishwa na usahihi wa utabiri wetu na asilimia 96.3 wameonesha kuzielewa taarifa hizo zinazotolewa na TMA hivyo kuzifikisha kwa jamii kwa lugha rahisiā. Alisema Dkt. Changāa.
Aidha, Dkt. Changāa ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wadau wa Maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa nchini na hivyo kuwezesha Mamlaka ya Hali ya Hewa kuendelea kuboresha huduma zake kwa kutoa utabiri mahususi kwa sekta mbalimbali nchini.
āKwa kuzingatia umuhimu wa huduma za hali ya hewa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuboresha miundombinu ya utoaji huduma za hali ya hewa ikiwemo ufungaji wa Rada za hali ya hewa na kuwajengea uwezo wataalam wa hali ya hewa, ambapo watumishi wapatao 97 wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wanaendelea na masomo ya elimu ya juu ndani na nje ya nchiā. Alisema Dkt. Changāa
Naye, mwanahabari kutoka Harvest FM, Bw. Yonna Mgaya alitoa mrejesho wa namna taarifa za hali ya hewa zimekuwa rahisi kupatikana kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na kufanikiwa kuzirusha zaidi ya mara mbili kwenye kituo chao. TMA inatarajia kutoa rasmi utabiri wa Msimu wa Mvua za Vuli 2025, tarehe 11 Septemba 2025, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
Watch, follow, and discover more trending content.