21/07/2025
Chuo Kikuu Cha UDOM Chasitisha Udahili Wa Wanafunzi Program Tisa.....
Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kimesitisha udahili wa wanafunzi katika programu tisa za shahada ya kwanza za ualimu kwa mwaka wa masomo 2025/2026, kikitaja sababu ya kufanya mashauriano na mamlaka za udhibiti.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa katika mitandao rasmi ya chuo hicho, programu zilizoathirika ni pamoja na Ualimu wa Sayansi, Saikolojia, Biashara, Sanaa, Mafunzo ya Habari na Mawasiliano, Elimu ya Watu Wazima na Maendeleo ya Jamii, Elimu ya Awali na Ushauri Nasaha, Utawala na Uongozi, pamoja na Mipango ya Sera na Usimamizi.
“Chuo kwa sasa kipo katika mashauriano na mamlaka husika ya udhibiti. Endapo kutatokea mabadiliko au taarifa mpya kuhusu tangazo hili, zitatolewa mara moja,” sehemu ya taarifa hiyo ilisomeka.
Kwa mjibu wa gazeti la "The Citizen", Makamu Mkuu wa Chuo cha Udom, Profesa Lughano Kusiluka amethibitisha kuwepo kwa mashauriano hayo, akisema chuo kiko kwenye majadiliano na wadau wote muhimu na kitaweka wazi taarifa kamili baada ya mchakato kukamilika.
“Hakuna haja ya kuwa na hofu. Tunafanya kazi kwa ukaribu na mdhibiti. Mara baada ya mazungumzo kukamilika, tutatoa mwongozo rasmi,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu sababu ya kusitisha programu hizo, Profesa Kusiluka amekataa kueleza kwa undani, akisema ni mapema mno kutoa maelezo na akatoa wito kwa umma kuwa na subira..
https://youtu.be/BU4gkV9pDeA