16/01/2026
Nyota wa kimataifa wa Senegal, Sadio Mané, amemstusha ulimwengu wa soka kwa kutangaza kuwa mchezo wa fainali ya AFCON utakaopigwa Jumapili dhidi ya wenyeji Morocco utakuwa wa mwisho kwake kushiriki mashindano hayo ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Mané ameweka wazi kuwa anatumaini kuiongoza Senegal kuibuka na ushindi na kutwaa taji hilo kwa mara nyingine ili kulipeleka jijini Dakar k**a zawadi ya mwisho kwa taifa lake kabla ya kuhitimisha safari yake kwenye mashindano hayo makubwa barani Afrika. Uamuzi huu wa Mané, mwenye umri wa miaka 33, unakuja baada ya kuisaidia timu yake kutinga fainali hiyo kwa kufunga bao la ushindi dhidi ya Misri katika nusu fainali.
Kauli hiyo ya Mané imewagusa mashabiki wengi wa soka barani Afrika, ikizingatiwa mchango wake mkubwa kwa Taifa la Senegal na soka la Afrika kwa ujumla tangu alipoanza kushiriki michuano hiyo mwaka 2015.
Fainali hiyo itakayopigwa katika uwanja wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat sasa itakuwa ya kihistoria kwa Mané, huku mashabiki wa "Simba wa Teranga" wakitarajia kumuona akimaliza safari yake ya AFCON kwa furaha na ubingwa wa pili katika historia ya nchi hiyo.
Kustaafu huku kwa Mané kwenye AFCON kunamaanisha hatashiriki michuano ijayo ya mwaka 2027 itakayofanyika katika nchi za Afrika Mashariki (Kenya, Uganda, na Tanzania).
Imedhaminiwa na