27/11/2025
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan, anatoa msukumo mkubwa kuhakikisha umeme unawafikia wananchi kote nchini kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Kauli hiyo ameitoa leo Novemba 27, 2025, wakati wa ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, ambapo ametaka kuona kazi inakamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa.
Amesema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa ufanisi mkubwa, hatua inayoliwezesha taifa kusonga mbele katika kujenga mfumo madhubuti wa upatikanaji wa nishati ya umeme.
Ndejembi amebainisha kuwa mradi huo mkubwa unatekelezwa kwa fedha za ndani, na hadi kukamilika kwake utagharimu takribani shilingi bilioni 556.
“Niwaagize TANESCO kuendelea kumsimamia Mkandarasi kuhakikisha kazi inakamilika kulingana na ratiba. Hatutaki kufika mwisho wa utekelezaji na kukuta mradi umekabidhiwa bila kukamilika,” amesisitiza Waziri Ndejembi.
Imeandikwa| Mwandishi Wetu
Tembelea http://epaper.ippmedia.com kusoma gazeti lako au wasiliana nasi 📞+255 745 -700 710 au 0677- 020 701 kwa maelezo zaidi.