18/08/2019
AMEEN KASHMIRI, MWANAJESHI MZALENDO WA TANZANIA ALIYEPITIA MENGI .
Historia ya Tanzania ina mengi na ina wengi ambao hawajazungumzwa, kiasi ambacho kuna mambo yakizungumzwa basi yanaweza kukusisimua na kukufanya ujisikie fahari sana kuwa Mtanzania.
Leo tunamzungumza Mzee wetu Mashuhuri Ameen Kashmiri. Askari Mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambaye historia ya maisha yake inatupa mafunzo na kutufahamisha mengi sana ambayo hatukuwa tukiyajua.
Ameen Kashmiri alizaliwa tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 1935 huko Mjini Tabora wakati huo kukijulikana k**a Jimbo la Magharibi, sehemu kubwa ya maisha yake ya utotoni ameyatumia huko wakati Baba yake ambaye alikuwa Mfanyakazi wa Shirika la Reli la Tanganyika alipokuwa kwenye Tawi hilo la Tabora.
Maisha ya Wafanyakazi wa wakati huo yalikuwa ya kuhamahama sana jambo ambalo lilimfanya Mzee Kashmiri asikae sana Tabora. Alihamishiwa Mkoani Dodoma, kisha Dar es salaam ambako nako hakukaa sana kabla ya kuhamishiwa Jimboni Tanga ambako ndipo sehemu alitumia sehemu kubwa ya maisha yake na ndipo Elimu na Mafunzo ya Mwanawe Ameen yalipopatikana.
Mwaka 1956 Bwana Ameen Kashmiri alihitimu Elimu yake ya Upili (Sekondari) katika Shule maarufu Jijini Tanga iliyojulikana kwa jina la Shule ya Karimjee (Sasa hivi ikijulikana k**a Shule ya Sekondari Usagara), ambapo kwa wakati wake alikuwa mmoja wa wanafunzi wenye uelewa mkubwa sana.
Tokea Shuleni yeye na baadhi ya Wenzake walivutiwa sana na habari na masimulizi ya Ushujaa, Ujasiri ya kusisimua ya wazee wengi wa Tanga ambao walikuwa Sehemu ya Jeshi la Wakoloni wa Kiingereza lililokwenda Burma na Somalia wakati ule wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na hivyo kuwafanya wavutiwe sana na wawe na wito wa kuwa maaskari Jeshi.
Mara tu alipomaliza Shule alifanya jitihada mbalimbali za kuomba kujiunga na Jeshi lakini mara zote alikataliwa. Pamoja na kuwa alionekana mweupe kwa rangi tofauti na Watanganyika wengine lakini bado alibaguliwa na Maofisa wa Kikoloni
>>ITAENDELEA