04/06/2026
ALIYETELEKEZWA AKIWA ANAUGUA UVIMBE MKUBWA USONI SASA AANZA MAISHA MAPYA
Binti mwenye umri wa miaka 22, Eliet (Neema) Rwechungura kutoka Bukoba, amepewa nafasi mpya ya maisha baada ya kupitia safari ngumu ya ugonjwa, upweke na changamoto za kifedha zilizokuwa zikihatarisha maisha yake.
Eliet alipoteza wazazi wake akiwa na umri wa miaka mitatu tu na kulelewa na baba mdogo huko Ifakara. Hata hivyo, mwaka 2022 alipofikisha miaka 18, mlezi wake huyo alifariki dunia na kumlazimu kurejea Bukoba kuishi na bibi yake.
Baadaye alipata mwenza na kuhamia naye mkoani Shinyanga. Wakiwa huko, Eliet alianza kuugua uvimbe mkubwa kwenye shavu uliosambaa hadi sehemu ya shingo, hali iliyobadilisha muonekano wake na kuathiri afya yake kwa kiasi kikubwa. Katika kipindi kigumu zaidi, mwenza wake alimtelekeza na kumwacha akiwa hana msaada wala makazi.
Akiwa amekata tamaa hospitalini, muuguzi mmoja wa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga aliguswa na hali yake na kuamua kumsaidia kwa gharama za vipimo. Matokeo yalibaini kuwa Eliet alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Ameloblastoma, uvimbe unaoshambulia mfupa wa taya na kusababisha uharibifu mkubwa wa uso.
Kutokana na hali yake, muuguzi huyo alimpa hifadhi na kushirikiana na madaktari wengine kuratibu matibabu yake. Baadaye alipatiwa rufaa kwenda Hospitali ya Bugando kwa ajili ya matibabu ya kibingwa, lakini changamoto ya fedha ilikuwa kikwazo kikubwa.
Kupitia juhudi za taasisi ya GH Foundation na michango ya Watanzania wenye moyo wa huruma, Eliet alipata fedha za matibabu na kufanikiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe pamoja na sehemu ya mfupa wa taya iliyoathirika.
Kwa sasa, hali yake inaendelea kuimarika na anaendelea na huduma za kliniki chini ya uangalizi wa wataalamu. GH Foundation pia imemkatia bima ya afya ili kuhakikisha anapata huduma za ufuatiliaji hadi atakapopona kikamilifu.
Hadithi ya Eliet ni ushahidi wa nguvu ya utu, mshik**ano na huruma ya Watanzania katika kuokoa maisha ya wenye uhitaji. Mchango wa madaktari, wauguzi, wafadhili na wananchi mbalimbali umegeuka kuwa tumaini jipya kwa binti ambaye wakati mmoja alikuwa amekata tamaa ya kuishi.
Hakika, pale ambapo matumaini yalionekana kufifia, upendo wa binadamu umeandika historia mpya ya maisha yake. โค๏ธ๐๐ฝ