27/06/2026
TFS YAWAAGA WASTAAFU 85, YASHUKURU MCHANGO WAO KATIKA UHIFADHI WA MISITU
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imewaaga rasmi watumishi wake 85 waliostaafu katika miaka ya fedha 2024/2025 na 2025/2026, huku ikisisitiza mchango wao mkubwa katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za misitu nchini.
Hafla hiyo ya kuwaaga wastaafu hao ilifanyika Juni 24, 2026 katika Ukumbi wa Mesuma jijini Dodoma, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na watumishi wa TFS.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Nkoba Mabula, alisema serikali inatambua mchango mkubwa uliotolewa na watumishi hao katika kuendeleza sekta ya misitu nchini.
Alisema uzoefu wao bado una thamani hata baada ya kustaafu, na kuwataka kuendelea kuwa mabalozi wa uhifadhi katika jamii wanazoishi.
“Wizara inatambua mchango wenu na taifa linajivunia uzalendo mlioonyesha. Kustaafu si mwisho wa jukumu la kulinda mazingira, bali ni mwanzo wa nafasi nyingine ya kutoa mchango,” alisema Mabula.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TFS, Luteni Mstaafu Chiku Abdallah Galawa, alisema hafla hiyo ni sehemu ya kuthamini na kusherehekea utumishi uliotukuka wa watumishi hao.
Alisema ni muhimu kwa watumishi waliopo kazini kujiandaa mapema kwa maisha ya baada ya kustaafu, akisisitiza kuwa kila mtumishi atafikia hatua hiyo.
Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, alisema TFS imekuwa ikiendesha mafunzo ya maandalizi ya kustaafu kwa watumishi wake ili kuwasaidia kuingia katika maisha mapya kwa ufanisi.
Alisema taasisi hiyo itaendelea kuthamini mchango wa wastaafu wake kwa kuwa ni sehemu muhimu ya historia ya mafanikio ya sekta ya misitu nchini.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa wizara, menejimenti ya TFS Makao Makuu, wakuu wa kanda na watumishi mbalimbali kutoka Makao Makuu na Kanda ya Kati.