
09/09/2025
JENEZA LA TAIFA (Sura ya Saba)
Mtunzi: Maundu Mwingizi
Januari 3, 1998, ikiwa ni Jumamosi ya mwisho kabla ya likizo kumalizika na kurejea shuleni kwa ajili kuanza darasa la pili, nilikwenda madrasa k**a ilivyo ada huku Dakota akienda mazoezini. Siku hiyo, madrasa hapakuwa na masomo, kwa sababu kulikuwa na kikao cha dharura baina ya wazazi na walimu, kilichofanyikia kwenye moja kati ya madarasa yaliyokuwa wazi, ambapo, ilikuwa rahisi kuwasikiliza wachangiaji mada kutokea katika darasa lingine tulilohifadhiwa kwa muda. Kikao kilitokana na baadhi ya watoto kukutwa wakichezea mipira ya kiume, waliyoiokota katika majalala ya jirani na mitaa ya Buguruni Danguroni.
“Binafsi naungana na hoja Mzee Bakari hapo. Hatupaswi kufanya subra kwa watu wanaotuharibia watoto wetu. Twendeni huko huko kwenye madanguro yao, tukawaadabishe wao pamoja na wateja wao,” mzazi mmoja, ambaye sikutambua sauti yake, alisikika akisema.
“Mimi, msisitizo wangu bado ni ulele. Hatutopungukiwa chochote kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi,” Bwana mmoja, aliyetajwa k**a Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, alisikika akisema. “Tukisema tujichukulie sheria mkononi, ndugu zangu, tutajiletea matatizo bure bileshi. Haya sawa, mwenzetu hapa amesema hiyo mipira ya kiume inatupwa ovyo majalalani na hao hao wanaojiuza, lakini hatuna ushahidi wa moja kwa moja kuwatia hatiani. Lau k**a watafanikiwa kujitetea, nasi tukashindwa kuthibitisha, basi wakitush*taki wallahi hatuchomoki. Tutajiingiza kwenye madhara makub…”
“Madhara gani makubwa kuliko maradhi wanayoweza kupata watoto wetu kwa kuchezea hiyo mipira–tena iliyokwishatumika!” Mchangiaji mwingine alisema. “Kuna madhara makubwa kuliko mmomonyoko wa maadili kwa vizazi vyetu unaosababishwa na upuuzi wa watu hawa wachache?”
“Ndugu zangu, nimekuwa nikifuatilia mjadala huu kwa utulivu ili kunasa hisia za kila mmoja,” Sheikh Ramiya, Imam wa Msikiti ulioko sanjari na madrasa yetu, alisikika akisema. “Ni kweli, kadhia hii inatokea kwa mara ya pili sasa. Mara ya kwanza, tulitoa taarifa Kituo cha Polisi, walakini hapakuwa na hatua madhubuti zilizochukuliwa. Sasa basi, pamoja na kwamba naafikiana na wachangiaji waliopendekeza kwenda kuwak**ata hao wahusika na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria, nachelea kupuuza angalizo tulilonasihiwa na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa hapa, k**a tahadhari tu ya kujiweka upande salama endapo lolote litatokea. Sasa je, tunaliwekaje hili ili tutimize azma yetu na tubaki salama?”
“Mimi nashauri hivi,” Ustadh Ahmada, mwalimu wetu wa madrasa, alisema. “Leo, saa mbili usiku, sote tuwe Kituo cha Polisi ili kutoa taarifa juu ya uchafu huu unaoendelea mtaani kwetu. Taarifa hiyo itaambatana na maelezo kwamba, muda huo huo, tunaelekea eneo la tukio kuwatia nguvuni wahusika. Kwa wingi wetu, bila shaka polisi wataiona hatari ya kutuacha twende peke yetu, na kwa hivyo watatufuata nyuma. Hapo tutakuwa tumepiga ndege wawili kwa jiwe moja; tutawak**ata wahusika tukiwa na ulinzi wa Polisi.”
Licha ya wachangiaji kadhaa kushauri namna nyingine za kulishughulikia jambo lile, rai ya Ustadh Ahmada ilikubalika zaidi na kupitishwa. Baada ya kikao kufungwa na watu kutawanyika, Ustadh Ahmada alikuja darasani na kuturuhusu turejee nyumbani. Ilikwishatimu saa kumi na mbili jioni.
Bupe alikuwa akipika wakati niliporejea nyumbani toka madrasa. Alikuwa amezungukwa na masufuria takribani sita, majiko mawili ya mkaa, ndoo za maji, pamoja na vitu vingine vidogo vidogo vyenye munasaba na mapishi. Pamoja na kutapanya vyombo vyote hivyo, alichokuwa akipika ni wali na maharage tu. Hilo likutoshe kufahamu Bupe alikuwa ni mpishi wa namna gani. Binafsi, sikumbuki kumwona, kabla ya siku hiyo, akiingia jikoni kupika.
“Shikamoo ma’mkubwa,” nilimsalimu.
“Marahaba, Chiku. Mzima?”
“Mzima,” nilimjibu na kuingia ndani.
Dakota aliyekuwa amesharejea nyumbani, nilimpita bila kumsalimia, akiwa amejilaza kwenye kochi sebuleni. Hatukuwa na utamaduni wa kusalimiana katika umri ule wa utotoni. Baada ya kumkosa mama chumbani, nilitoka na kumwuliza, “Dakota, mama yuko wapi?”
“Sijamwona.”
Nikamfuata Bupe hapo nje alipokuwa anapika, “Eti ma’mkubwa, mama yuko wapi?”
“Mama bado hajarudi,” alisema huku akinitazama usoni. Sauti yake yenye kitetemeshi ilivyosikika ni k**a anaongelea ndani ya maji. “Kuna nini?”
Nilimweleza habari niliyoisikia madrasa. Bupe ni mtu wa kudharau na kupuuza mambo. Huwa hajali chochote. Unaweza kutumia kila lugha kumtahadharisha na jambo la hatari, lakini maneno yako yote yakaingilia sikio moja na kutokea sikio lingine. Lakini taarifa hiii mpya, ilipoingia sikioni mwake, ilikita kwenye ubongo wake na kugoma kutoka. Papo hapo alinyanyuka na kuanza kuingiza vyombo ndani, kisha akatupakulia chakula na kuondoka akituacha tunakula.
Haikupita hata nusu saa, tukiwa tunamaliza kula, tulisikia kelele na purukushani za watu barabarani. Nilikimbilia chumbani kwa mama na kuchungulia dirishani. Watu walikuwa wakikimbia kuelekea bondeni, mitaa ya Buguruni Danguroni. Nilirudi sebuleni kumwambia Dakota kilichokuwa kikiendelea huko nje, nikijaribu kukihusianisha na kile nilichokisikia kwenye kikao cha wazazi.
“Twende tukaangalie,” Dakota alisema, akijua fika tulishakatazwa kutoka nje usiku, achilia mbali kwenda kwenye vurugu k**a hizo.
Mpambano mkali baina ya moyo na akili uliibuka ndani yangu. Kimoja kilitaka niende na kingine kikitaka nibaki nyumbani. Mara kwa mara ndani ya ubongo wa kila mtoto, huibuka mpambano baina ya umakini na upumbavu. Na mara nyingi upumbavu ndiyo hushinda. Hivyo, pamoja na kufikiria hatua ambazo mama atatuchukulia, endapo atakuta tumeacha nyumba bila mtu na kukimbilia huko Danguroni kushangaa vurugu, hatukujali.
“Twende, lakini tuwahi kurudi,” nilisema. Kabla hata sijamaliza kusema, tayari Dakota alikuwa ameshasimama nje ya mlango.
Tulifunga mlango na kushika njia. Dakota alikuwa mwenyeji wa mitaa ya Danguroni zaidi yangu, hivyo, nilimfuata nyuma bila kuuliza uhakika wa njia alizonipisha. Badala ya kutumia njia ya mzunguko, ambayo mama yangu hutumia, tulikatiza kichochoro cha kwanza, kisha tukanyoosha hadi kichochoro cha pili, kilichotuchukua hadi mtaa wa Danguroni.
Watu walikuwa wametawanyika huku na kule kushuhudia uk**ataji. Pamoja na idadi kubwa ya watu, ambapo kila mmoja alikuwa na jasho lake, bado harufu ya udi wa Danguroni ilisikika wazi wazi. Akina dada wanaojiuza walikuwa wanatoka kwenye vyumba vyao na kutimua mbio kukwepa polisi, huku baadhi yao wakik**atwa. Mtu wa kwanza kumwona akiwa amedhibitiwa na wak**ataji ni huyu mwanamke mnene, mweupe, aliyevaa gauni fupi na jepesi bila kitu ndani. Alifanana sana na yule tuliyemwona akimwingiza mwanaume chumbani mwake siku ile ya kwanza tulipokuja kwa Bupe. Alikuwa amek**atwa pamoja na mteja wake, bwana mmoja wa kati ya miaka 45 mpaka 50.
Jirani na chumba alichok**atiwa huyu mwanamke mnene, palikuwa na mwanamke mwingine mwembamba, mrefu, aliyegoma kuk**atwa baada ya kutolewa chumbani alikokuwa na mteja wake. Alikuwa akipigana na vijana waliokuwa wamekunja kanzu zao viunoni. Zilipiganwa ngumi za bila mpangilio hadi askari walipofika kumchukua wenyewe. Watu walikuwa wakishangilia na kuzomea kwa wakati mmoja.
Wote waliok**atwa walipelekwa kwenye karandinga ya polisi, iliyokuwa imeegeshwa mbele ya ile nyumba ambayo Bupe alimwambia mama yangu kuwa Dakota alikuwa akilala kwa rafiki yake. “Twende kule,” Dakota alisema, akinionesha kwa kidole kule lilipokuwa gari la polisi.
Kwenye karandinga ya polisi mlikuwa na wanawake kadhaa wanaojiuza pamoja na wateja waliok**atwa nao. Wakati tukiliambaa gari na kuhamia upande wa pili, ndipo nikamwona mama yangu akiwa miongoni mwa wanawake waliowekwa chini ya ulinzi. Ilikuwa picha mbaya sana machoni mwangu. Kwanza sikuamini, lakini baada ya kutulia kwa sekunde kadhaa, nilijihakikishia kuwa ni yeye. “Mama! Mama!” nilimwita ili walau nimpungie mkono, lakini sauti yangu ilimezwa na kelele zilizokuwa zimehanikiza eneo hilo.
Alikuwa ameinamisha kichwa chini k**a anayekwepa watu kumtambua. Nilijaribu kumwita tena bila mafanikio. Dakota alinishika mkono na kunivuta ili tuondoke eneo hilo ambalo ghasia na msongamano vilishtadi kweli kweli. Tuliondoka na kwenda kusimama mbele ya ile nyumba aliyokuwa akilala Dakota.
“Chiku!” Nilisikia sauti ambayo si ngeni masikioni mwangu ikinipigia kele. “Chiku! We Dakota!”
Tulipogeuka kufuata mwelekeo wa sauti tukakutanisha macho na Bupe, aliyekuwa ndani ya uzio wa nyumba hiyo, akichungulia kila kinachoendelea hapo barabarani. Tulimfuata tukiwa tumenywea k**a p**o lililotiwa mwiba.
“Mmefuata nini huku,” Bupe alisema, huku akimchapa kofi Dakota na kisha akafuata kwangu. Sikuwahi kumwona Bupe amekasirika k**a siku ile.
Alituondoa eneo la tukio na kuturejesha nyumbani muda huo huo. Njia nzima alikwenda anatukemea na kutusukuma k**a vibaka. Laiti k**a tungekuwa hatujala, siku hiyo tungelala na njaa, kwani alipotufikisha tu nyumbani, alitoa amri kila mmoja apitilize chumbani kulala kisha yeye akatoka tena. Sidhani k**a siku hiyo Bupe alilala. Alikuwa akizunguka k**a pia. Alitoka na kurudi nyumbani kila baada ya nusu saa. Na aliendelea na utaratibu huo kwa saa kadhaa hadi pale nilipopitiwa na usingizi.
*****
Jumatatu asubuhi, ikiwa ni siku ya tatu bila kumwona mama nyumbani, nish*tuka usingizini na kumwona mtu akiwa amesimama chumbani mwetu, mbele ya masanduku ya nguo. Nilishindwa kumtambua kwa haraka kutokana na mwanga uliopenya kwenye dirisha lililofunguliwa. Alikuwa Bupe. Alikuja kuniamsha kwa ajili ya kwenda shule.
Ilikuwa ni Jumatatu ya kufungua shule baada ya likizo ya mwezi wa kumi na mbili kutamatika. Lakini kulikuwa na haja gani ya kuniamsha kwa mtindo ule wa kufungua madirisha, niliwaza. Alishindwaje kuniamsha k**a alivyokuwa akituamsha mama?
Asubuhi hiyo niliota ndoto ya ajabu: Niliingia chumbani nikitokea bafuni kuoga. Mama yangu hakuwemo chumbani, lakini mezani palikuwa na kioo kidogo cha kujitazama. Siku zote mama alikificha mbali kioo chake ili nisikiguse, akidai kuwa mtoto akianza kupenda kujitazama kwenye kioo ataharibika tabia mapema. Niliangaza kulia na kushoto kisha nikakichukua na kujitazama. Badala ya kujiona sura yangu, nilimwona mtu mmoja ambaye sikumtambua kwa haraka akiwa amempiga kabali mama yangu. Pembeni yake alikuwapo Baruti, mtoto wa mama Sandra, akimpiga na kumng’oa nywele mama yangu huku akipambana kumpokonya madaftari yangu ya shule. Mvulana mwingine alikuwa amesimama upande wa pili wa barabara, akifuatilia kwa mbali mwenendo wa tukio zima na kutoa maelekezo ambayo, sikuweza kumwelewa alikusudia kumhami mama yangu au kuwawezesha akina Baruti. Kila nilipojaribu kukiweka kioo vizuri ili nimtambue, aligeuka pembeni na kujificha uso. Niliendelea kukigeuza kioo kushoto na kulia hadi nilipomnasa sura yake. Alikuwa ni Dakota. Kwa namna alivyokuwa akijificha uso ili nisimtambue ni dhahiri alikuwa anashirikiana na akina Baruti kumdhuru mama yangu. Kwa nini Dakota anafanya hivi? nilijiuliza.
Nilijaribu kufumba tena macho ili kujaribu kuimalizia, lakini Bupe akanisemesha. “Haya muda wa shule, Chiku.”
Nilifumbua tena macho na kumtazama hali ya kuwa mawenge ya usingizi yakiniandama. “Shikamoo ma’mdogo,” nilimsabahi.
“Marahaba.”
“Mama ameshaachiliwa?”
“Atarudi leo.”
Namna alivyotamka utadhani mama alikuwa safarini kurejea nyumbani. Ingawaje alijua fika kwamba, mimi na Dakota tunafahamu kuwa mama amek**atwa na polisi, hakutaka kabisa kututhibitishia hilo kwa kauli wala vitendo. Hata alipokuwa akimpelekea chakula polisi tangu alipok**atwa, hakutuambia anapeleka wapi chakula. Kufikiria tu kwamba, mama yangu pamoja na wahalifu wengine, alikuwa chini ya polisi kulitosha kunipa homa. Nilinyanyuka kitandani na kutembea hadi dirishani. Nikasimama na kutazama nje. Anga lilikwishakuwa pevu likinururishwa na weupe wa mawingu ya asubuhi.
Siku hiyo shuleni, kinyume na shauku na matarajio yetu, hatukuingia darasani. Badala yake tulipokelewa na zoezi la usafi wa shule, lililoanza asubuhi hadi mchana tuliporuhusiwa.
“Eti mama yako amek**atwa na polisi?” Sandra aliniuliza tulipokuwa tukirejea nyumbani toka shuleni.
“Nani kakwambia?” nilimwuliza, ingawaje nilikuwa na hisia kwamba atakuwa amesikia kwa mama yake.
“Nimewasikia akina Edna wakati tunafanya usafi.” Edna ni mtoto wa rafiki yake Bupe, anayeishi kwenye ile nyumba tulipomkuta Bupe akichungulia siku mama alipok**atwa.
Nilitamani kumwuliza, wamesema amek**atwa kwa kosa gani? Lakini nilijionya, k**a wameshajua kuwa amek**atwa, bila shaka watakuwa wanaijua sababu pia. Hivyo, sikukubali wala sikukataa. Nilibaki kimya nikitazama hewani ilhali fedheha ikinitafuna moyoni.
Sandra aliendelea kunitazama akitaraji majibu. Nilipokutanisha naye macho, nikageuka pembeni kuficha msawajiko wa uso wangu. “Amek**atwa kweli?” aliniuliza tena.
“Nilidhani ma’mkubwa ndiye amekwambia!” nilisema– nikimaanisha mama yake. Hakunijibu. Nami sikuendeleza majadala.
Siku iliyofuata, kwa mara ya kwanza, tulifika shuleni kwa kuchelewa. Bupe hakutuamsha kwa wakati. Wanafunzi wote walikwishaingia madarasani. Tuliingia darasani kwa kunyata na kusita, tukihofia kumkuta mwalimu. Tulipoingia darasani, wanafunzi wote walitugeukia mlangoni, wakidhani mwalimu ameingia.
“Humu ndani kuna watu wananuka udi wa Danguroni,” James alisema huku akijiziba pua kwa mkono.
Karibu nusu nzima ya darasa walicheka na kutuangalia. Kwa kawaida, udi hunukia. Hivyo, kitendo cha James kusema kuna watu wananuka udi wa Danguroni, baada ya kutuona tukiingia darasani kilibeba dhihaka dhidi yetu; mimi na Dakota. Hatukujali. Tukaketi kwenye madawati yetu.
Haikuchukua muda mrefu, Mwalimu Rehani Mkonongo aliingia darasani na kujitambulisha k**a mwalimu wa darasa. Alivaa shati jeupe la mikono mirefu na suruali nyeusi ambayo sehemu kubwa ya mapajani ilitapakaa vumbi la chaki. Zoezi la kwanza lilikuwa ni kutupanga kwenye madawati. Utaratibu ulikuwa ni ule ule wa kuchanganya jinsi. Mimi na Bijou tulipangwa pamoja na Bilal Kaisi. Papo hapo Bilal alijiinamia na kuanza kulia.
“Unalia nini, Bilal?” Mwalimu Rehani aliuliza huku akikunja mikono ya shati lake na kufanya bangili yake ya shaba katika mkono wa kushoto ionekane.
“Mimi sitaki kukaa dawati moja na huyu,” alisema–akiniashiria mimi.
“Kwa nini hutaki kukaa naye?”
“Atanifundisha tabia mbaya,” alisema kwa sauti ya chini, akijifuta machozi kwa kiganja cha mkono. “Mama yake am…” Kabla hajalifikisha mwisho neno lake, kicheko cha haja kililipuka baina ya wanafunzi wenzangu na kumfanya Bilal kusita.
Mwalimu Rehani alinyanyua uso na kulitazama darasa na kimya kikatanda. “Mnacheka nini?”
Hakuna aliyejibu.
“Haya endelea,” alisema huku akimgeukia Bilal. “Atakufundisha tabia gani?” Bila aliinamisha kichwa chini. “Sasa k**a hujibu, utakaa hapo hapo na wenzako. Na nikikuta umebadili nafasi utajuta kuzaliwa.”
Siku iliyofuata tulipoingia darasani, James aliwahi kuketi kwenye nafasi yangu, akifuatiwa na Bilal kisha Bijou. Hata aliponiona hakutaka kunipisha. Kila nilipotaka kumwambia anipishe kwenye nafasi yangu nilihisi vinyweleo vya hofu vikinitutumka.
“Naomba kukaa,” hatimaye nilisema, huku nikilainisha mdomo wangu kwa ulimi.
“Mnf! Mnf!” James alifanya k**a anayejiziba pua kwa kutumia mdomo huku akitoa pumzi nzito–ishara ya harufu mbaya. Papo hapo Bilal naye alijiziba pua kwa kutumia kola ya sweta lake.
James aliendelea kuketi pale pale ilhali nami nikisimama vile vile hadi aliposikia mwalimu akiingia darasani ndipo alinyanyuka haraka na kwenda kwenye dawati lao nami nikaketi. Mwalimu alipotoka baada ya kumaliza kufundisha, James alirudi tena na kuniamuru nimpishe kwenye nafasi yangu. Nilijihisi machozi yakinilenga machoni.
“We mtoto wewe,” Dakota, aliyekuwa ameketi kwenye moja kati ya madawati ya safu ya kulia, alisema huku akimnyooshea James kidole cha onyo. “Mwache mwenziyo akae.”
“Nani ni mtoto?” James alisema, akiniacha na kumfuata Dakota. “Unataka mchezo?” Alikunja ngumi tayari kwa kupigana. “Njoo nikuue! Njoo!”
Dakota alimtazama James wakati wanafunzi wengine wakichekelea. “Miye sitaki ugomvi na mtu. Mwalimu akitukuta tunapigana atatuchapa,” alisema.
“Poa. Tukitoka basi… saa saba… pale mwembeni,” James alisisitiza huku akikunjua ngumi na kunigeukia. “Na wewe ujiandae.”
Sikuwa na cha kujibu. Nilikosa raha kabisa. Nilitamani hata kumwomba msamaha japo sikulijua kosa langu.
***** Kabla ya kujiuliza ni ipi hatma ya Chiku na Dakota dhidi ya James Manonga, kwanza tujiulize ni nini hatma ya Maya (Mama Chiku) aliyeko mikononi mwa polisi? Lakini pia, ni ipi hatma ya shughuli iwaingiziayo kipato akina Bupe? TUKUTANE TENA kesho saa 12:30 jioni.