
05/04/2025
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kutegemea kupata umeme wa uhakika baada ya Mradi wa kufua umeme kutoka Bwawa la Julius Nyerere uliokuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa na Watanzania kukamilika rasmi.
Waziri Biteko ameyasema hayo leo April 5, 2025 baada ya kutembelea Mradi huo akiwa ameambatana na Mawaziri ambao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mha. Hamadi Masauni.
Amesema hivi sasa mitambo yote tisa inafanya kazi ambapo amefafanua kuwa kukamilika kwa Mradi huo kumechangiwa na maono ya Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye aliupokea Mradi ukiwa katika asilimia 33 ya utekelezaji wake na ndani ya kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake ameweza kuukamilisha Mradi.
Katika hatua nyingine Mhe Dkt Doto Biiteko amelishukuru Shirika la umeme Tanzania TANESCO kwa utekelezaji wa Mradi kwa kiwango cha kimataifa na kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Mha. Gissima Nyamo-Hanga kwa usimamizi na jitihada zake katika kusimamia miradi mbalimbali ya umeme.
Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere umegharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 6.5 ambapo mpaka sasa serikali imeshalipa zaidi ya asilimia 99.5.