03/10/2026
NCHI IKO SALAMA KWA CHAKULA – YASEMA KAMATI YA BUNGE
Tabora📍
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imesema usalama wa nchi unaanza na usalama wa chakula, hivyo wananchi hawapaswi kushangazwa na mabadiliko makubwa yanayofanywa na Serikali katika kuwezesha miradi ya Umwagiliaji.
Kamati hiyo imeeleza kuwa jitihada za Serikali katika kuwekeza kwenye miradi ya Umwagiliaji zinalenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na kujidhatiti katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, hali inayoiwezesha pia kuihakikishia dunia kuhusu uwezo wake wa uzalishaji.
Akizungumza katika muendelezo wa ziara ya kukagua miradi ya umwagiliaji inayosimamiwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Mjini, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika, amesema Tanzania ni salama na msingi wake ni uhakika wa chakula.
Mwanyika amesema nchi imekuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula kwa matumizi ya ndani na hata nje ya nchi, jambo linaloifanya kuwa tegemeo kwa baadhi ya nchi za Ukanda wa SADC.
Ameeleza kuwa ili miradi hiyo iendelee kutoa manufaa kwa muda mrefu, ni muhimu itunzwe kupitia rasilimali za ndani ikiwemo kodi na tozo, ili kuhakikisha inakuwa endelevu na yenye tija kwa wananchi.
“Si rahisi kusema mradi huu ni wetu halafu matengenezo yake apeleke mtu mwingine, si sawa,” amesema Mwanyika akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa pamoja katika kulinda miundombinu hiyo.
Aidha, ametoa angalizo kuwa miradi inayojengwa na Serikali inahitaji utunzaji wa karibu, na kwamba wananchi wanapaswa kuelewa mchango wao kupitia ada na tozo mbalimbali ili kuhakikisha miundombinu hiyo inabaki katika hali nzuri muda wote.
Mwanyika ameongeza kuwa miradi ya umwagiliaji inaendeshwa kwa ufanisi na thamani ya fedha inaonekana kulingana na kazi zinazofanyika, akibainisha kuwa miradi hiyo inagusa moja kwa moja maisha ya wananchi na kutoa matumaini makubwa ya kiuchumi.