05/01/2026
Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, leo Jumatatu Januari 05, 2026, anatarajiwa kuongoza zoezi la utoaji wa msaada wa kisheria bure mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi, sambamba na kuelekea siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tangu alipoingia madarakani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Katiba na Sheria, zoezi hilo linalenga kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kisheria, ikiwemo migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, malezi na ulinzi wa watoto, upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa, pamoja na changamoto nyingine zinazohitaji ufumbuzi wa kisheria.
Huduma hizo zitatolewa kupitia kliniki maalum za msaada wa kisheria zitakazohusisha wataalamu wa sheria pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara. Wananchi watapatiwa elimu ya kisheria, ushauri wa kitaalamu, pamoja na mwongozo wa hatua za kuchukua kulingana na changamoto zao.
Aidha, mkutano wa pamoja wa kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi unatarajiwa kufanyika katika Viwanja vya Stendi ya Zamani, Manispaa ya Morogoro, ambapo wananchi watapata fursa ya kuwasilisha hoja na changamoto zao moja kwa moja kwa wataalamu wa sheria na viongozi wa taasisi husika.
Mbali na utoaji wa huduma kwa wananchi, Dkt. Homera anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi katika taasisi za haki zilizopo mkoani Morogoro kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu yao, kusikiliza changamoto na kutoa maelekezo yatakayoboresha utoaji wa huduma za kisheria.