11/09/2026
Mwanachama wa CHADEMA na Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano, Odero Charles Odero, ametoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia msiba wa kuondokewa na mume wake, huku akimuombea marehemu apumzike mahali pema.
Odero amewataka viongozi wa CHADEMA kutumia kipindi hiki cha msiba kufika na kutoa pole kwa Rais Samia na familia yake, akisisitiza kuwa misiba ni sehemu inayowaunganisha watu na kuwawezesha kusahau tofauti zao.
Amesema kauli ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, ya kuwataka viongozi na wafuasi wa chama hicho kufikisha salamu zake za pole kwa Rais Samia na familia yake inaonesha uungwana, ubinadamu na moyo wa maridhiano.
Odero amekumbusha pia kuwa Rais Samia aliwahi kutuma salamu za pole kwa CHADEMA wakati wa msiba wa mmoja wa waanzilishi wa chama hicho, Edwin Mtei. Hivyo, amewataka viongozi wengine wa CHADEMA, wakiwemo waliopo Zanzibar, kutumia nafasi hiyo kufika na kuhani msiba.