Snapstz

Snapstz if you can't make it good, make it big.

05/07/2025

27/06/2025
Maisha ya CHADEMA bila MBOWEHatimaye chama cha CHADEMA kimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kabisa kuyaishi maneno yanayo ak...
30/01/2025

Maisha ya CHADEMA bila MBOWE

Hatimaye chama cha CHADEMA kimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kabisa kuyaishi maneno yanayo akisi maana halisi ya jina la chama chao. Kwa kuendesha chaguzi kubwa katika ngazi ya chama kitaifa na kudhihirisha demokrasia ya kweli mbele ya umma wa Tanzania.

Hakika Demokrasia ilishuhudiwa na kuonekana ikitendeka katika uchaguzi huu wa kihistoria uliogubikwa na kampeni zilizojaa maneno lukuki ya shombo. Hasa kutoka kwa wagombea wakuu wa nafasi ya uwenyekiti, ambapo halmanusra wagawane mbao baada ya chama kupasuka vipande vipande.

Uchaguzi huu ulikuwa ni tukio la kivutio kwa wengi hasa kwa wapenzi wa siasa za vyama vingi hapa nchini Tanzania. Kiasi cha kumshawishi Baba Askofu wa Dayosisi ya Karagwe ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Benson Bagonza kuamua kuutolea uchambuzi wenye hisia kali. USHINDI WA TUNDU LISSU NA KUSHINDWA KWA FREEMAN MBOWE KWENYE UCHAGUZI WA MWENYEKITI WA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA).

Kamati ya Uchaguzi wa CHADEMA ilimtangaza Lissu kuwa mshindi kwa kura 513 za wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama. Akimwangusha Mbowe aliyekuwa anatetea kiti alichokikalia kwa miaka 21 na Odero Charles. Mbowe alipata kura 482 huku Odero akiambulia kura moja.

Kufuatia ushindi huo wa Lissu na timu yake iliyokuwa inamuunga mkono katika uchaguzi huo, akiwamo Bw. John Heche aliyemshinda Ezekia Wenje katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara. Askofu Bagonza ameibuka na andishi lifuatalo:

Ninaandika kupongeza. Sina pole za kutoa.

Ninawapongeza Mwenyekiti Tundu Lissu na Makamu wake, mtani wangu Heche. Hata mimi siamini k**a mmeshinda lakini sina pa kukata rufani. Mwaka huu nina bahati sana. Makamu wote wa vyama vikubwa ni watani wangu: Steven Wasira na John Heche. Kuna nini hapa? Ninajiteua kuwa mpatanishi siku wakigombana.

Ninampongeza Freeman Mbowe. Ameshinda kuliko alivyoshindwa. Ametufundisha sote. Kukubali matokeo hutokana na mchakato uliojaa uhuru, uwazi na haki. Tuzo ya MO Ibrahim inamhusu lakini iwe na bahasha nzito, siyo kupewa ubao tu.

Ninampongeza Mwakajoka na Mnyika kwa kusimamia vizuri uchaguzi usiku kucha. Hakuna kazi mbaya k**a kusimamia uchaguzi. Mwulizeni Mheshimiwa Jaji Mstaafu, Mzee Damian Lubuva! Baada ya pongezi, nibwabwaje haya:

Mbowe siyo Mugabe kwa sababu Mugabe hakuwahi kushinda wala kushindwa uchaguzi. Daima aliamua apate kura ngapi.

Mbowe siyo Mugabe wala wale wote waliowahi kukaa madarakani muda mrefu. Nilikuwapo wakati wa Mwalimu Julius Kambalage Nyerere; k**a angegombea 1985, angeshinda. Nilikuwapo mwishoni mwa Mzee Rukhsa - Rais Ali Hassan Mwinyi. Mkapa – Mzee wa Ukweli na Uwazi. Kikwete – Mzee wa Msoga. Mwamba kabisa JPM wa “hapa kazi tu” (Atake Asitake), na hata sasa nipo na Mama Kizimkazi, Chifu Hangaya, Rais Samia Suluhu Hassan. Wote hawa wangegombea baada ya vipindi vyao kwisha, bado wangeshinda! Mbowe ameshindwa na amekubali matokeo. Yeye ni zaidi ya “Bwana Darasa” la siasa nchini.

Mbowe si Mugabe. Jamani! Si rahisi kumshinda aliye kitini. Mjinga mmoja wa chama kingine kaniandikia, “Mwamba kaamua tu kumlegezea mropokaji; angeamua kubaki wangemfanya nini?”
Nami nikamjibu, “waulize waliowahi kuamua kubaki. Toka kujadiliwa na Baraza la Mawaziri hadi kutojadiliwa na Baraza la Madiwani!” Huko si kuanguka ni kuporomoka. Mbowe kathibitisha umwamba wake.

Tundu Lissu siyo Trump. Wanafanana ukali wa maneno si ujinga wa kisiasa. Wote walipigwa risasi, zikawaongezea kura zao. Wapinzani wa Lissu ndani ya CHADEMA wakapuuza risasi zake na kumwongezea huruma. Lissu ni hukumu isiyo na rufani kwa watawala wanaotumia risasi badala ya hoja. Rudisheni risasi mfukoni, nendeni shule mjifunze hoja. Wamarekani walitumia risasi, sasa wanaongozwa na “kichaa mstaarabu”.

Tundu Lissu siyo Trump. Kwa Trump mihimili inajitegemea na ina nguvu. Hapa kwetu, mihimili inamtegemea Lissu aiseemee na kuisimanga. Mmemsahau Spika Makinda? “Mwanangu Lissu, ebu tusaidie tuondoke hapo jamani”. Ninatamani Tulia atulie mbele ya Makinda apate twisheni ya kufanya kazi na Lissu.

Tundu Lissu na Freeman wameelewana. Wapambe wao wamenuniana. Tatizo lilikuwa moja. Tundu Lissu aliwamudu na kuwaendesha wapambe; Mwamba wapambe walimmudu na kumwendesha. Wote wawili ni somo kwetu: wapambe wanaweza kukuambia wakati gani kuingia uwanjani (Lissu), lakini hawawezi kukuambia wakati gani utoke uwanjani (Mwamba).

Mbowe amefuta makosa yake yooote ya miaka 21 kwa kubonyesha kitufe kimoja tu: kukubali matokeo. Lissu kachukua mkopo mkuuubwa wenye riba kubwa wakati kazungukwa na vibaka. Atamudu kurejesha mkopo huu? Neno kwa Mbowe: Ukistaafu, USTAAFU. Neno kwa Lissu: Mahaba ya kutongozea na kuolea ni tofauti na mahaba ya kuishi Maisha ya NDOA.

Wanachadema na Watanzania: Msiyemtaka kaja. Mliyemtaka kaja. Tuna taifa la kutunza na kustawisha. Mambo yetu hayako sawa. Walio madarakani wananung'unika. Walio nje wananung'unika. Wageni wananung'unika. Wawekezaji wananung'unika. Tusiridhiane ili hali iendelee. Turidhiane kuondoa hali hii. Watawala wa zamu, msipuuze watu kulala sakafuni Mlimani City. Kuna kitu ndani yao.
Wako wenye shaka na Lissu. Nami nimo. Tulio na shaka tuna bahati moja: hatuhitaji kumharibia Tundu Lissu. Yeye ana uwezo mkubwa wa kujiharibia. Tumwombee.

Huu ni mwaka wa uchaguzi. Kwa CCM kumaliza mkutano wake na CHADEMA kuhitimisha uchaguzi wa ndani, taifa linaweza kuwa tayari limempata rais, chama tawala na chama kikuu cha upinzani. Penye CCM waweza kuweka CDM na penye CDM waweza kuweka CCM bila kuathiri maana ya nisemacho.

HAKI inaunganisha, DHULUMA inaligawa taifa.

Salaam nyingi toka barafu za milima ya Ufaransa na Ujerumani.

Ni mimi Lwakalinda Benson Kalikawe Bagonza.

Baa la Moto L.A.Mlipuko wa janga la Moto wa nyika katika jiji la Los Angeles. Jiji la pili kwa ukubwa nchini Marekani. U...
15/01/2025

Baa la Moto L.A.

Mlipuko wa janga la Moto wa nyika katika jiji la Los Angeles. Jiji la pili kwa ukubwa nchini Marekani. Umewaacha watu wengi katika msh*tuko mkubwa ambao hawajawahi hata kufikiri kiwango cha maafa kilicho fikiwa mpaka kufikia sasa.

Ni moto ambao umekuwa vigumu kudhibitiwa na unaendelea kuteketeza sehemu za Los Angeles, na kusababisha vifo vya takriban 25. Na kuharibu mamia ya majumba zaidi ya elfu kumi na mbili, na kulazimisha zaidi ya watu 140,000 kuyakimbia makazi yao.

Licha ya jitihada za wazima moto, miale mikubwa ya moto wa nyika Inaendelea kushika kasi. Huku hali ya hewa na athari za mabadiliko ya tabianchi zikitarajiwa kuendelea kuzidisha moto siku zijazo.

Madhara ya Moto wa Nyika L.A.

Zaidi ya watu 140,000 wameyakimbia makazi yao, huku wengi wao wakionekana kubeba vitu kiasi vya thamani walivyo jaliwa kubeba. Lakini kikubwa zaidi ni kuokoa uhai wao na kuamini kuwa mali zitaendelea kutafutwa tu.

Polisi wana endelea kabiliana na vibaka waliojitokeza kwa wingi wakioneka kuvalia mavazi ya askari waokoaji. Na kuingia katika majumba ya watu kwa madhumuni ya Kutaka kuiba vitu mbali mbali vya thamani.

Kwa upande mwingine, moto wa nyika wa Sunset ambao ulikuwa ukiathiri eneo maarufu la Hollywood Hills umeanza kupungua kasi. Japo bado haujadhibitiwa kabisa ila kwa sasa watu wameruhusiwa kubaki katika maeneo yao huku wakichukuwa tahadhali.

Majumba takribani 2,000 yameshuhudiwa kuharibiwa, ikiwemo nyumba, shule, na biashara katika Barabara maarufu ya Sunset Boulevard. Na mandhari za mtaa huo zimeharibiwa kabisa.

Miongoni mwa watu maarufu waliopoteza nyumba zao ni Leighton Meester na Adam Brody. walioshiriki tu tuzo za Golden Globe siku chache zilizopita, pamoja na Paris Hilton.

Huduma za Mafuta ya umeme yamekatwa katika maeneo mengi ya jiji, na msongamano wa magari umeongezeka.

Mnyukano wa wanasiasa.

Mzozo wa kisiasa kuhusu ufanisi wa maandalizi ya jiji la Los Angeles wakati wa dharura umeibuka baada ya kugundulika. Kuwa mabomba ya baadhi ya wazima moto hayakuwa na maji, jambo ambalo limeibuliwa na rais mteule wa Marekani, Donald Trump.
Lakini katika jimbo la jirani ya Pasadena, Mkuu wa Zimamoto Chad Augustin. Alisema eneo hilo lilichelewa kidogo kwa uokozi kutokana na maji ya kuzima moto kukosa shinikizo la kurusha maji maghorofani. Lakini Masuala yote yametatuliwa, alisema.

Alihusisha suala la kupungua kwa shinikizo “pressure” na vyombo vingi vya moto kuvuta maji kwa wakati mmoja. Pamoja na kupoteza kwa shinikizo la kupunguza nguvu ya kurusha maji ya kuzima moto.
Rais Joe Biden naye pia amemshutumu Rais mteule Bwana Trump na wenzake wa Republican. Kwa kutounga mkono uthibiti wa matendo yanayo athiri mfumo wa Hali ya Hewa hivyo kusababisha athari za tabia nchi.

Tathmini ya kiwango cha uharibifu mpaka sasa.

Kwa sasa, moto angalau tano unawaka katika maeneo mapana, kulingana na maafisa wa moto wa California, Alhamisi asubuhi.
Eneo la Palisades: Moto wa kwanza kutokea Jumanne na kuwa moto wa nyika mkubwa zaidi katika eneo hilo. Unaweza kuwa moto mbaya zaidi katika historia ya jimbo. Umechoma sehemu kubwa ya ardhi, ukifunika zaidi ya ekari 17,200, ikiwemo eneo la kifahari la Pacific Palisades.

Eneo la Eaton: Moto huu umeathiri sehemu ya kaskazini ya Los Angeles, ukiteketeza miji k**a Altadena. Ni moto wa pili kwa ukubwa katika eneo hilo, ukiteketeza karibu ekari 10,600.

Eneo la Hurst: Lilio kaskazini mwa San Fernando, lilianza kuteketea siku ya Jumanne usiku. Na limeongezeka hadi ekari 855, ingawa wazima moto wamefanikiwa kwa kiasi kidogo kudhibiti moto huo.

Eneo la Lidia: Moto wa nyika huu ulianzia Jumanne alasiri katika eneo la milima la Acton kaskazini mwa Los Angeles. Na umefikia ukubwa wa ekari karibu 350 mamlaka zinasema umeweza kudhibitiwa kwa asilimia 40.

Eneo la Sunset: Moto huu ulianzia Jumanne jioni katika Hollywood Hills, ukikua hadi ekari 20 chini ya saa moja. Umezunguka ekari 43 lakini sasa umeanza kupungua.

Moto wa awali wa Woodley na Olivas sasa umeweza kudhibitiwa, kulingana na maafisa wa moto wa eneo hilo.

Historia ya Moto wa Nyika L.A.

Ingawa upepo mkali na ukosefu wa mvua vinachochea kwa kiasi kikubwa cha kuzuka kwa moto. Wataalamu wanasema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanabadilisha hali ya kawaida na kuongeza uwezekano wa milipuko mikali ya moto k**a hii.

"Mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo joto kali, ukame wa muda mrefu, na anga inayohitaji mvua. Imekuwa kichocheo muhimu katika kuongezeka kwa hatari na ukubwa wa madhara ya moto maeneo ya magharibi mwa Marekani." inasema Idara ya Kitaifa ya Oceanic na Hali ya Hewa.

Baada ya msimu wa joto kali na ukosefu wa mvua katika miezi ya karibuni, California iko katika hatari kubwa.

Msimu wa moto kusini mwa California kawaida kuanza kutoka mwezi Mei hadi Oktoba, lakini gavana wa jimbo hilo, Gavin Newsom. Alieleza mapema kuwa milipuko ya moto imekuwa tatizo la karibu kila mwaka.

mkuu wa kikosi cha zima moto cha California Bw. Acuna alisema kuwa Moto wa Palisades ni wa tatu katika miaka 30 iliyopita ambapo moto mkubwa ni huu wa Januari.

Mabadiliko ya Tabia nchi.

Maafisa wanataja upepo mkali na ukame katika eneo hili. Ambao umeifanya mimea hasa nyasi kuwa kavu kabisa na kuwa kichocheo kikubwa cha muendelezo wa moto.

Athari zinazo wezekana kusababishwa na mabadiliko ya tabianchi pia zinatajwa - ingawa mazingira halisi bado hayajulikani.

Zaidi ya asilimia 95 ya majanga ya moto wa nyika katika eneo hili inaanzishwa na shughuli za kibinadamu. Kulingana na David Acuna, mkuu wa kikosi cha zima moto cha California.

Ingawa maafisa hawajatoa maelezo kamili kuhusu chanzo cha moto huu wa sasa.

Kipengele muhimu kilichotajwa katika kuenea kwa moto ni upepo wa Santa Ana, ambao unapuliza kutoka bara kuelekea pwani. Kwa kasi ya zaidi ya maili 60 kwa saa (97 km/h). Inaaminika kuwa upepo huu umekuwa ukifanya moto kuzidi kuteketeza misitu na majumba.

YANGA yazindukia kwa Mkapa.Mtindo maarufu ulio “trendi” hapa mjini wa 'Gusa Achia Twenda Kwao' ambao wananchi wana tamba...
07/01/2025

YANGA yazindukia kwa Mkapa.

Mtindo maarufu ulio “trendi” hapa mjini wa 'Gusa Achia Twenda Kwao' ambao wananchi wana tamba nao. Hasa hapa nyumbani katika ligi ya NBC.

Hatimaye mtindo huo umefufua matumaini ya Yanga kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili mfululizo. Baada ya kuinyoosha vilivyo TP Mazembe kwa mabao 3-1. Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

TP Mazembe ndiyo ilianza kupata bao la kuongoza baada ya Chadrak Boka kutoa “boko” dakika 16 tu ya mchezo. Kwa kucheza “sliding tackle” ya hovyo. Na kusababisha “faul” ndani ya kumi na nane na kuzaa penalti iliyotolewa na mwamuzi Ahmad Imtehaz Herreralall kutoka Mauritius. Mkwaju huo uwekwa kimiani na kipa Badara Faty aliyemtungua Diarra Djigui aliyerejea uwanjani kwa mara ya kwanza kutoka kwenye majeraha.

Tukio hili liliwapa matumaini Mazembe kuwa wamesha uchukuwa mchezo. Kwani walikuwa waki kumbuka ahadi ya mamilioni ya fedha waliyoahidiwa kwa kila bao ambalo wangefunga. Na kuipa timu hiyo ushindi kutoka kwa Rais wa klabu hiyo, Moise Katumbi.

Ile 'Gusa Achia Twenda Kwao' ya Yanga ilifanya kutumika vizuri eneo la kati. Lililokuwa likiongozwa na Khalid Aucho, Mudathir Yahya akisaidiana na Pacome Zouzoua na Aziz KI. Kutengeneza mashambulizi na kufanikiwa ndani ya dakika tisa tu kupata kona mbili za haraka. Japo hazikuzaa matunda kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Mazembe.

TP Mazembe walionekana kucheza kwa mtindo wa kujilinda zaidi huku waki tengeneza mashambulizi ya kushtukiza. Huku wananchi wakizidisha hasira mithili ya moto uliomwagiwa mafuta ya petroli.

Ilipotimia dakika 32, Boka aliyeng'ara katika beki ya kushoto alikokota mpira na kummegea pasi ya upendo Clement Francis Mzize. Aliyeipatia Yanga Goli kali kwa kuachia shuti la umbali wa mita karibia 20 akimtungua Faty aliyeruka kulidaka bila mafanikio.

Dakika mbili baadae Prince Dube na Stephane Aziz Ki walipoteza nafasi mbili za wazi ambazo zilipotea kwa kukosa umakini. Vinginevyo Yanga wangeenda mapumziko wakiwa mbele.

Kipindi cha pili Yanga ilirudi na kasi zaidi ya 'Gusa Achia Twenda Kwao' iliyowa nyamazisha kabisa wageni. Baada ya Aziz KI kufunga bao la pili akimalizia pasi ya Khalid Aucho. Aliyekuwa na mpira ndani ya lango la TP Mazembe kwa kumpiga tobo kipa Faty aliyetokea kumkabili.

Bao hilo lilifungwa dakika ya 56 kabla ya Mzize kukamilisha hesabu kwa kufunga bao la tatu dakika ya 60. Akipokea pasi ya Prince Dube na kuwa bao la pili kwake katika mchezo huo na hatua ya makundi.

Yanga ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Aziz Ki, Aucho na Pacome Zouzoua. Nafasi zao zilichukuliwa na Keneddy Musonda, Duke Abuya na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wote waliingia kipindi cha pili cha mchezo.

Kuendeleza ile 'Gusa Achia Twenda Kwao' ili kuulinda ushindi wa mabao 3-1. Huku TP Mazembe nayo ikibadilisha wachezaji wanne ambao hawakuweza kubadilisha matokeo ya mchezo huo.

Matokeo hayo yamerejesha tumaini kwa Yanga ya kufuzu robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo. Baada ya kusaliwa na mechi mbili, ikiwamo moja ya ugenini dhidi ya Al Hilal inayoongoza msimamo wa kundi hilo. Na ile ya mwisho dhidi ya MC Alger ya Algeria.

Al Hilal ina pointi tisa na MC Alger ina nne sawa na Yanga, lakini timu hizo mbili zimecheza mechi tatu. Tofauti na Yanga na Mazembe inayoburuza mkia ikiwa na pointi mbili zilizocheza michezo minne kila moja.

Yanga Sc V TP Mazembe

32' Mzize 15' Faty (P)
56' Aziz Ki
60' Mzize

Address

Dar Es Salaam

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Snapstz posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Business

Send a message to Snapstz:

Share