01/03/2021
MBWA KUTUMIKA KUGUNDUA WAGONJWA WA COVID19
MBWA waliofunzwa nchini Finland wana uwezo wa kugundua wagonjwa walio na maambukizi ya virusi vya corona (Covid-19).
Mbwa hao waliopewa mafunzo maalum wamekuwa wakitumika katika viwanja vya ndege nchini humo tangu Septemba, kudhibiti abiria kwa sababu ya Covid-19. Kulingana na matokeo ya awali, kiwango cha usahihi ni kati ya asilimia 95 na asilimia 100.
Baada ya ukaguzi wa Covid-19 ambao unafanyika ndani ya dakika moja, abiria huruhusiwa kuendelea na safari zao kwa kutegemea na matokeo ya vipimo vya mbwa hao.
Katika mchakato wa ukaguzi, abiria hufuta shingo zao kwa vitambaa vya kufyonza, kisha vitambaa hivyo huwekwa kwenye makopo ambapo baadaye mbwa huja kufanya ukaguzi kwa kunusa upande wa pili wa kuta za makopo hayo.
Ikiwa matokeo yanaonyesha kuwa na maambukizi, abiria hupelekwa kwenye kitengo cha huduma za afya katika uwanja wa ndege.