16/01/2026
Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeandaa kambi maalum ya matibabu ya kisasa ya upasuaji wa kuondoa mawe kwenye figo kwa wagonjwa wenye changamoto hiyo kwa kutumia njia ya kisasa ya mionzi ya laser, ambapo kambi hiyo itafanyika kuanza tarehe 21-23 januari, 2026.
Daktari Bingwa wa Upasuaji Mfumo wa Mkojo Dkt. Hamis Isaka ameeleza kuwa kutokana na huitaji wa huduma hiyo kwa watu wengi, hospitali imeamua kufanya matibabu hayo ili kuhakikisha wananchi wananufaika na uwekezaji mkubwa uliyofanywa na Serikali katika sekta ya afya .
Amefafanua kuwa huduma ya kuvunja mawe kwenye figo kwa kutumia mionzi ya Lesar ni matibabu ambayo humsaidia mgonjwa kupata maumivu kidogo ,kutokuwa na kovu wala kukatwa ambapo mgonjwa atakaa wodini kwa muda mchache takribani siku moja hadi mbili.
Kwa mujibu wa Dkt. Isaka, huduma hiyo inahusisha wagonjwa wenye mawe kwenye figo madogo hadi ya kati, wagonjwa ambao dawa hazikusaidia, wanaoogopa upasuaji mkubwa, wagonjwa wenye uzito mkubwa au matatizo ya damu na wanaopata mawe ya figo mara kwa mara.
Aidha , Dkt. Isaka ameeleza namna ya kuzuia mtu kupata mawe kwenye figo ni pamoja na kunywa maji mengi angalau lita 3 kwa siku, kupunguza matumizi ya chumvi nyingi, kupunguza nyama nyekundu kupita kiasi, kula matunda na mbogamboga, kufanya mazoezi na kufanya uchunguzi wa mara kwa mara.