12/10/2023
Serikali imesimamisha leseni zote Nchi nzima za Kampuni ya Nadoyoo Mineral Trading kufuatia kukamatwa kwa mmoja wa wahusika wa Kampuni hiyo akitorosha dhahabu takribani kilo 4.3 zenye thamani ya zaidi ya
shilingi Milioni 562,288,207.
Hayo yamesemwa Usiku wa kuamkia leo Oktoba 11, 2023 na Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari Wilayani Kahama baada ya kukamatwa kwa mfanyabiashara huyo "Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan haitakubali kuona watu wachache wanajihusisha na vitendo hivi viovu vya kutorosha madini. Nataka niwaambie, tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote tutakayemkamata akijihusisha na utoroshaji wa madini” amesema Mh. Mavunde.
“Ninapoingia Wizara ya Madini mwezi mmoja uliopita nilisema, ukitaka kufahamu sura yangu nyingine basi jaribu kutorosha madini. Sasa basi, kuanzia leo mtu yeyote atayekamatwa kwa kosa la kutorosha madini, tutakwenda kusimamisha leseni zake zote Nchi nzima wakati tukisubiri hukumu ya vuombo vya sheria, na iwapo mahakama itabaini mhusika ana hatia, tutakwenda kuchukua hatua kali ikiwemo kufuta kabisa leseni zote na kuhakikisha hatajihusisha tena na biashara ya madini nchini” aliongeza Mhe. Mavunde.
Sambamba na hilo, Mhe. Mavunde alitoa wito kwa wafanyabiashara wa madini kuwa wazalendo kwa kufuata taratibu zilizopo na kulipa tozo, ada na kodi mbalimbali ili kuiwezesha Serikali kupata mapato na kuendelea kuimarisha huduma kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara, umeme, afya na elimu.
Pia, Mheshimiwa Mavunde alionesha utayari wa kutenga siku na kukaa pamoja na wafanyabiashara wa madini ili kwa pamoja wamweleze hasa ni nini wanadhani inaweza kuwa ni changamoto kubwa inayopelekea baadhi yao kufikia hatua ya kujihusisha na vitendo vya utoroshaji madini, hatua ambayo anaamini itasaidia Serikali kuchukua njia sahihi kushughulikia suala hilo.
Vilevile, Mheshimiwa Mavunde alieleza bayana kuwa pamoja na hatua kali
za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watoroshaji wa madini, pia madini
yote yatakayokamatwa yatahifadhiwa na Serikali.