16/07/2025
WAKAZI KIN'GAZI WACHANGAMKIA MAUNGANISHO YA MAJI
๐ Kin'gazi A, Dar es Salaam
Watendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya mtaa Kin'gazi A, Kata ya Kwembe, Wilaya ya Ubungo wamegawa vifaa vya maunganisho mapya ya maji kwa wananchi mbalimbali.
Lengo ni kuwezesha wananchi kuunganishwa moja kwa moja na mtandao wa majisafi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Usambazaji Maji Dar es Salaam ya Kusini (Bangulo) ambao umekamilika kwa gharama ya Shilingi 36.9 bilioni.
Vifaa ambavyo vimetolewa ni pamoja na mabomba, koki, dira za maji na vifaa vya usalama vya kuunganisha maji majumbani.
Meneja wa DAWASA โ Kinyerezi, ndugu Roberts Mugabe amesema zoezi hilo linalenga kuhakikisha wananchi wanaanza kupata huduma ya majisafi kwa urahisi na kwa wakati ambapo wateja 130 tayari wamekabidhiwa vifaa vya maunganisho mapya na zoezi la kuunganisha huduma linaendelea.
โMradi huu wa Bangulo umeleta mabadiliko makubwa kwa maeneo ya Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam. Tunataka wananchi waanze kuona matokeo chanya kwa vitendo, na ndiyo maana tumeanza kugawa vifaa ili kuharakisha maunganisho ya maji,โ amesema ndugu Roberts.
Ndugu Roberts ameongeza zoezi la maunganisho ni endelevu kwani hadi sasa mkoa wa kihuduma umepokea maombi takribani 400 ambapo hadi sasa tayari wateja 130 wamekabidhiwa kwa ajili ya kuunganishwa huku taratibu zikiendelea kwa ajili ya waliobaki na wanaoendelea kuwasilisha maombi.
Kaimu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kin'gazi A, ndugu James Frank ameishukuru DAWASA na Wizara ya Maji kwa kuwaleta wananchi wake kwenye mstari wa mbele wa maendeleo, akibainisha kuwa maji ni kichocheo kikubwa cha afya na ustawi wa jamii.
"Kwa hili DAWASA inastahili pongezi kwa kusogeza huduma kwa wananchi, nitoe rai kwa wananchi kuendelea kufika ofisini kuomba huduma kwani sisi tuko kwa ajili ya kuwahudimia," ameeleza ndugu James.
Mkazi wa Kin'gazi A, Jolicia Ngowi ameipongeza DAWASA kwa kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumtua mama ndoo kichwani.
"Tumehangaika na changamoto ya upatikanaji wa maji kwa muda mrefu ambapo ilitulazimu kununua maji kwa bei ghali au kuchota sehemu zisizo salama. Niwapongeze DAWASA kwani sasa napata maji baada ya kukamilisha taratibu ndani ya muda mfupi," amesema ndugu Jolicia.
Mradi wa usambazaji maji Dar es Salaam ya kusini (Bangulo) ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kimkakati kitaifa inayotekelezwa kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi. Mradi huu unalenga kunufaisha majimbo matano ya uchaguzi ya Ukonga, Segerea, Ubungo, Ilala na Ubungo ambapo takribani wananchi 450,000 watanufaika na mradi huu.