27/07/2025
Katika ajali ya kusikitisha iliyotokea leo kwenye eneo la mteremko wa Mbembel, kati ya Nzovwe na Lyunga jijini Mbeya, lori lenye namba za usajili T 576 CAK pamoja na tela namba T 121 CAY, lililokuwa limebeba shehena ya mbolea limehusika kwenye ajali baada ya kushindwa kuhimili mfumo wa breki.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Ofisa Oparesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mbeya, Gervas Fungamali, lori hilo liliteleza kwenye mteremko na kugonga magari kadhaa madogo, yakiwemo mabasi mawili ya abiria. Ajali hiyo imesababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine kadhaa.
Fungamali amesema kuwa kikosi cha uokoaji kiliweza kuutoa mwili wa marehemu kutoka eneo la tukio na kuwaokoa majeruhi, ambao idadi yao kamili itatangazwa baada ya taratibu za uhakiki kukamilika.
Tukio hili linaongeza wito kwa madereva na wamiliki wa magari makubwa kuhakikisha magari yao yanakuwa na mifumo bora ya breki, hasa wanapopita kwenye maeneo yenye miinuko mikali k**a ya Mbeya.