
19/05/2025
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Mambo ya Ndani na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchukua hatua za haraka kwa wanaotumia mitandao na teknolojia vibaya, akikemea pia wingi wa Wanaharakati kutoka nje ya nchi wanaojaribu kuingilia mambo ya ndani ya Tanzania na kutaka kuivuruga amani.
Rais Samia amesema hayo Jijini Dar es salam leo May 19, 2025 wakati akizindua Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 (Toleo la 2024), ambapo amesema hatotoa nafasi kwa watovu wa adabu kutoka nje ya nchi kuja kujaribu kuvuruga amani, utulivu na usalama uliopo nchini Tanzania.
“Tusiwe shamba la Bibi kwamba Mtu anaweza kuja Tanzania akasema analolitaka, lipo Tanzania halipo, Watu wakajisemea tu, tumeanza kuona mwenendo wa Wanaharakati ndani ya Ukanda huu kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu huku, sasa k**a kwao wameshadhibitiwa wasije kutuharibia, tusitoe nafasi walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika ni hapa kwetu, niwaombe Vyombo vya Ulinzi na Usalama kutotoa nafasi kwa Watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kutovuka hapa kwetu, hapana”
“Nimeona clip kadhaa za kunisema, nipo bias na nini, ninalofanya ni kulinda nchi yangu na ndiyo wajibu wangu niliopewa, kwahiyo hatutotoa nafasi kwa kiumbe yeyote kuja kutuvurugia hapa awe yupo ndani ama anayetoka nje”
Katika maelezo yake, Rais Samia ameitaka Wizara na Maafisa wanaohusika kutoa ufafanuzi kuhusu yale yanayosemwa na Wanaharakati na Watu mbalimbali, kukanusha ama kuchukua hatua za haraka ikiwa yanayosemwa yana ukweli kuhusiana na sekta zao mbalimbali.