09/08/2026
MISUNGWI CUP YAGEUKA FURSA KWA WAJASIRIAMALI LUDETE
MISUNGWI CUP imeendelea kuwa chachu ya fursa za kiuchumi kwa wajasiriamali wadogo katika Kata ya Ludete, baada ya wafanyabiashara waliokuwa wamejitokeza kuuza bidhaa zao kupata nafasi ya kuwahudumia mashabiki waliofika kushuhudia michezo ya robo fainali.
Furaha na shangwe za mashabiki katika Uwanja wa Ludete Sekondari hazikuishia kwenye burudani ya soka pekee, bali mashindano hayo yamegeuka kuwa fursa kwa wajasiriamali wadogo kuuza bidhaa zao na kuongeza kipato.
Katika hatua ya kuonyesha umuhimu wa kuwaunga mkono wajasiriamali hao, Diwani wa Kata ya Ludete na mwandaaji wa mashindano hayo, Jumanne Misungwi, alifika katika eneo walilokuwa wakifanyia biashara na kununua bidhaa mbalimbali, kisha kuzigawa bure kwa wananchi waliokuwepo uwanjani
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Jumanne Misungwi amesema lengo ni kuunga mkono juhudi za wajasiriamali wadogo pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wao
Amesema michezo haipaswi kuangaliwa k**a burudani pekee, bali inaweza pia kuwa sehemu ya kuibua na kuunganisha fursa za kiuchumi kwa wananchi, hususan vijana na wajasiriamali wadogo.
Hatua hiyo imepokelewa kwa furaha na mashabiki waliokuwepo uwanjani, huku ikionyesha namna mashindano ya Misungwi Cup yanavyoweza kuwa jukwaa la michezo na wakati huo huo kuchochea shughuli za kiuchumi ndani ya Kata ya Ludete.