22/08/2025
TOSCI YAAGIZWA KUSHIRIKIANA NA TAKUKURU KUDHIBITI MBEGU FEKI NCHINI
Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imetakiwa kushirikiana kwa karibu na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kudhibiti uuzaji na usambazaji wa mbegu feki kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa kwa wakulima na maendeleo ya kilimo nchini.
Agizo hilo limetolewa leo Agosti 22, 2025 na Waziri wa Kilimo nchini Hussein Bashe jijini Dodoma, wakati akizindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI).
Waziri Bashe amesema kuwa ni lazima TOSCI na TAKUKURU waimarishe ushirikiano wao ili kuwabaini na kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wote wanaojihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinaathiri maendeleo ya kilimo kwa wakulima nchini.
Kwa mujibu wa Wizara ya kilimo, mahitaji ya mbegu bora kwa mwaka nchi Tanzania ni tani 127,650 katika mwaka 2025/2026, ambapo uzalishaji wa mbegu bora ndani ya nchi unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 63,526.54 hadi tani 90,000 huku upatikanaji wa mbegu bora nchini unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 79,700.62 hadi tani 105,000.