02/01/2026
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameweka mezani dhamira yake bila kuficha chochote kuelekea michuano ya Kombe la Mapinduzi, huku wekundu hao wakijiandaa kushuka dimbani kesho kuivaa Muembe Makumbi City.
Akizungumza na wanahabari mapema leo, Barker alisema wazi kuwa Simba haijaenda Zanzibar kwa matembezi, bali kwa lengo moja kuu—kunyakua taji la michuano hiyo.
Kocha huyo aliongeza kuwa mashindano hayo yatakuwa fursa muhimu kwake kuwapima wachezaji wake na kuona maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya safari ndefu ya msimu kuendelea.
“Tumekuja na dhamira ya kuwa mabingwa, lakini pia ni jukwaa muhimu kwangu kuwafahamu wachezaji wangu kwa undani zaidi. Hii ni sehemu ya maandalizi ya mashindano makubwa yanayokuja, ikiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika,” alisema Barker kwa kujiamini.
Simba iliyopo Kundi B, itaanza kampeni yake kesho Januari 3, 2026 kwa kumenyana na Muembe Makumbi City kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja. Baada ya hapo, Januari 5, 2026 itashuka tena dimbani kuikabili Fufuni katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi.
Mara baada ya Kombe la Mapinduzi kumalizika, macho ya Simba yatageukia Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo inasubiriwa na kibarua kizito dhidi ya Esperance de Tunis. Mchezo wa kwanza utapigwa ugenini Januari 23, 2026 kabla ya marudiano nyumbani Januari 30, 2026.
Ikumbukwe kuwa katika mechi mbili za awali za Ligi ya Mabingwa, Simba imeambulia vichapo viwili mfululizo na kwa sasa inashika mkia wa Kundi D, jambo linaloifanya michuano ya Mapinduzi kuwa fursa muhimu ya kurejesha morali na kuusuka upya utambulisho wa kikosi hicho.
NB: USISAHAU KU-SUBSCRIBE CHANNEL YA WATANI WA JADI YOUTUBE
*********************************************