22/07/2025
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, leo amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la kisasa la ghorofa nane la Kituo cha Jiomolojia Tanzania, TGC, linaloendelea kujengwa katika jiji la Arusha.
Mradi huo, unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 33, unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Madini na taasisi ya TGC, na unatarajiwa kuwa kitovu cha shughuli za uongezaji thamani madini ya vito, tafiti za kisayansi, pamoja na biashara ya madini nchini.
Katika ziara hiyo, Waziri Mavunde alipokea taarifa ya maendeleo kutoka kwa Mhandisi Julian Mosha wa Kampuni ya Skywards Lumocons Joint Venture, pamoja na msimamizi wa mradi kutoka TGC, Jumanne Nshimba.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Mavunde alisema mradi huo ni wa kimkakati kwa sababu unakusudia kuwa na madarasa ya mafunzo, karakana, maabara ya kisasa ya madini, mabweni ya wanafunzi, na ofisi za chuo, huku pia ukiwa kituo cha One Stop Centre kwa wafanyabiashara wa madini.
Kwa upande wao, viongozi wa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini mkoani Arusha akiwemo Mwenyekiti wa AREMA Ndg. Alfred Mwaswenya na Mwenyekiti wa CHAMATA Ndg. Jeremia Kituyo, wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu ujenzi wa jengo hilo ambalo wamesema litaongeza fursa za ajira, ujuzi, na urahisi wa kufanya biashara katika mazingira salama na ya kitaalamu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Kenani Kihongosi, amesema kuwa mradi huo utasaidia kuongeza mzunguko wa uchumi wa mkoa na kuiweka Arusha k**a kitovu cha madini ya vito Afrika Mashariki.
Jengo hilo linatarajiwa kukamilika ndani ya muda wa mkataba, na serikali imesisitiza dhamira yake ya kuifanya Tanzania kuwa kinara wa biashara na uongezaji thamani wa madini barani Afrika.