21/12/2025
DKT. MWIGULU AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI LINDI–RUANGWA–NACHINGWEA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, leo Desemba 21, 2025 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa Maji wa Lindi–Ruangwa–Nachingwea katika Kijiji cha Chimbila A, Wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi.
Mradi huo wa maji unaochota maji kutoka Mto Nyangao uliopo Wilaya ya Lindi, unatekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). Mradi utanufaisha jumla ya vijiji 56, ambapo vijiji 34 vipo Wilaya ya Ruangwa, vijiji 21 Wilaya ya Nachingwea na kijiji 1 Wilaya ya Lindi.
Ujenzi wa mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 119 na hadi sasa umefikia asilimia 67% ya utekelezaji. Mradi ulianza kutekelezwa Februari 2023 na unatarajiwa kukamilika Juni 2026 kwa hatua ya kwanza. Hata hivyo, ifikapo Februari 2026 baadhi ya vijiji vitaanza kupata huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza baada ya uwekaji wa jiwe la msingi, Mhe. Dkt. Mwigulu amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa maendeleo yaliyofikiwa yanazidi kiwango cha fedha kilichotolewa hadi sasa.
“Hivi ndivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anavyotaka kuona kazi za maendeleo zikifanyika. Hapa tumeona asilimia ya utekelezaji ni kubwa kuliko fedha zilizotolewa hadi sasa,” amesema Dkt. Nchemba.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwigulu ametumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Kassim Majaliwa, kwa kuasisi mradi huo na kufuatilia kwa karibu upatikanaji wa fedha za utekelezaji wake, hatua ambayo imewezesha mradi kufikia hatua ya kuridhisha.