24/12/2025
HABARI: Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, ametoa mwito wa kusitishwa kwa mapigano ulimwenguni kote wakati wa sikukuu ya Krismasi.
Akiwa katika makazi yake ya mapumziko ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma mnamo Disemba 23, 2025, Papa ameeleza hamu yake ya kuona ulimwengu ukisherehekea kuzaliwa kwa Mwokozi katika mazingira ya utulivu na amani.
Katika ujumbe wake huo kuelekea Disemba 25, Papa ameeleza kusikitishwa kwake na msimamo wa Urusi ambao unaonekana kukataa ombi la kusitisha mapigano nchini Ukraine kwa ajili ya siku hiyo takatifu.
“Ninatoa tena wito wangu kwa watu wote wenye mapenzi mema, kuheshimu siku ya amani, angalau katika sikukuu ya kuzaliwa kwa Mwokozi wetu," alisema Papa, huku akisisitiza kuwa ni jambo la kuhuzunisha kuona milio ya risasi ikiendelea wakati wa sherehe za amani.
Kiongozi huyo ameweka wazi kuwa lengo lake ni kuona dunia ikipata angalau saa 24 za amani kamili, bila kujali ukubwa wa mizozo iliyopo.
Mwito huu unakuja wakati hali ya usalama nchini Ukraine ikiendelea kuwa tete, ambapo taarifa za kijeshi zinaashiria kuwa majeshi ya Ukraine yamelazimika kujiondoa katika mji mmoja muhimu upande wa Mashariki kufuatia mashambulizi makali kutoka kwa Urusi.
Kuhusu uwezekano wa yeye kuitembelea Ukraine kufuatia mwaliko wa Rais Volodymyr Zelensky, Papa Leo XIV amesema "anatumai hivyo," ingawa amekiri kuwa bado ni vigumu kupanga tarehe rasmi ya safari hiyo kwa sasa.
Papa alikutana na Rais Zelensky mapema mwezi huu wa Disemba, katika juhudi za kutafuta suluhu ya kudumu ya kidiplomasia katika eneo hilo.
Follow Us
Istagram
Facebook
Twitter
Youtube .