14/11/2025
Ziara ya wataalamu wa misitu kutoka Jimbo la Hunan, nchini China, imeingia hatua ya pili baada ya ujumbe huo kutembelea Makao Makuu ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yaliyopo Itega, Dodoma. Lengo la ziara hiyo ni kuweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya uhifadhi, utafiti na utalii wa kiikolojia kati ya taasisi hizo mbili.
Mazungumzo yaliyofanyika jana yalihitimishwa kwa makubaliano ya awali ya kuandaa makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya TFS na Idara ya Misitu ya Hunan. Makubaliano hayo yataainisha maeneo mahsusi ya ushirikiano, yakiwemo tafiti za pamoja, ubadilishanaji wa wataalamu na kukuza utalii wa mazingira asilia, hususan katika hifadhi za misitu.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Kamishna wa Uhifadhi wa Misitu, Prof. Dos Santos Silayo, alisema makubaliano hayo yatatoa dira mpya ya ushirikiano wa kimataifa katika kulinda misitu, kukuza tafiti za pamoja na kuendeleza utalii unaohusisha jamii katika shughuli za uhifadhi.
“Tumeafikiana kuandaa mfumo wa ushirikiano wa muda mrefu utakaowezesha kubadilishana wataalamu, teknolojia za uhifadhi, na kukuza tafiti za pamoja za utalii wa kiikolojia. Hii ni fursa kubwa ya kuimarisha diplomasia ya uhifadhi na kulinda misitu yetu kwa manufaa ya vizazi vijavyo,” alisema Prof. Silayo.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Ujumbe wa Wachina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu ya Hunan, Jianga Rui, alisema Serikali ya China imeweka dhamira ya kuanzisha uhusiano wa kindugu kati ya hifadhi za misitu za nchi hizo mbili. Alisema dhamira hiyo inalenga kuimarisha uelewa wa pamoja kuhusu uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya utalii wa misitu.
“Tumevutiwa na mfumo wa Tanzania wa usimamizi wa hifadhi na namna jamii inavyoshirikishwa katika uhifadhi. Tunataka kujifunza kutoka kwenu na kuanzisha miradi ya pamoja itakayokuza uhusiano wa kirafiki na kukuza utalii wa mazingira asilia,” alisema Jianga Rui.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa taratibu za ndani za mkoa wa Hunan, ushirikiano huo utapitia njia za kidiplomasia. Hivyo, baada ya kurejea China, timu yake itawasilisha taarifa rasmi kwa mamlaka husika ili kura.