29/07/2025
NI MARUFUKU WAGENI KUFANYA BIASHARA HIZI TANZANIA !
Serikali ya Tanzania imepiga marufuku wageni kufanya biashara 15 ndogo na za kati nchini humo, hatua ambayo inaweza kuwalazimisha wafanyabiashara wengi kutoka Kenya wanaofanya biashara na wanaotaka kuanzisha biashara nchini humo kuweka pembeni malengo yao.
Kwa mujibu wa notisi iliyotolewa na waziri wa viwanda na Biashara wa Tanzania, Selemani Saidi Jafo, biashara hizo ziko chini ya sekta ya madini, utalii, kilimo, mazingira na teknolojia.
Biashara hizo ni pamoja na kuhamisha fedha kwa njia ya simu, ukarabati wa simu za mkononi na vifaa vya kielektroniki, biashara za saluni (isipokuwa zinafanywa hotelini au kwa madhumuni ya utalii), usafi wa nyumba, ofisi na mazingira, na uchimbaji mdogo wa madini.
Nyingine ni pamoja na huduma za posta na vifurushi, kuongoza watalii, kuanzisha na kuendesha stesheni za redio na TV, majumba ya makumbusho na maduka ya kudadisi, udalali wa biashara na mali isiyohamishika.
Wageni pia wamepigwa marufuku kufanya kilimo, shughuli za ununuzi wa mazao, umiliki au uendeshaji wa mashine au vifaa vya kamari, isipokuwa ndani ya kasino, na umiliki na uendeshaji wa viwanda vidogo. Mgeni atakayepatikana akifanya biashara hizi atatozwa faini ya hadi Tsh10 milioni (Ksh502,927) na kifungo kisichozidi miezi sita.
Kwa mujibu wa waziri huyo, raia yeyote wa Tanzania ambaye atapatikana akiwasaidia wageni kufanya biashara hizo atatiwa hatiani na kuadhibiwa kwa kifungo cha miezi mitatu jela, pamoja na faini ya Tsh5 milioni (Ksh251,463).
Tangazo hilo linakuja siku chache baada ya Wizara ya Fedha ya Tanzania, katika notisi ya mapema mwezi huu, kutangaza kwamba wageni wanaonuia kusafiri kuja nchini, kuanzia mwaka ujao, watatakiwa kulipa karibu Tsh. 115,000 sawa na Ksh5,700 za Kenya ili kununua bima ya lazima ya kusafiri kwa watalii. Kwa mujibu wa Wizara, hatua hiyo inanuia kuondoa mzigo kwenye mifumo ya afya ya umma nchini.
Maagizo hayo yamewasaza wananchi kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); hata hivyo, wasafiri wanaoingia nchini kutoka nje ya EAC/SADC bado wanaweza kutakiwa kulipa ada hiyo.
Bima hiyo ilikuwa sehemu ya ajenda ya mwaka wa fedha wa 2025/2026 lakini ilisogezwa hadi Januari 2026 ili kutoa nafasi zaidi ya mashauriano na wadau.
MWANDISHI Fazul Khalid