19/10/2025                                                                            
                                    
                                                                            
                                            MHAGAMA AWAFUNDA WATENDAJI KATA NA VIJIJI UKUSANYAJI WA MAPATO
Na Ahadi Mtweve, Moshi DC
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Ndugu Shadrack Mhagama, ameongoza kikao kazi maalum kilichowahusisha Watendaji wa Kata na Vijiji kutoka maeneo yote ya wilaya, kwa lengo la kufanya tathmini ya hali ya ukusanyaji wa mapato na kujadili mikakati ya kuongeza ufanisi katika usimamizi wa fedha za umma.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhagama aliwataka watendaji kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uwazi na kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma. Alisisitiza kwamba jukumu la ukusanyaji wa mapato ni la msingi katika uendelevu wa shughuli za maendeleo ya wananchi.
“Nawasihi watendaji wote muwe waaminifu katika kukusanya mapato ya serikali. Fedha hizi ni za wananchi na zinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Ni jukumu letu kuhakikisha kila senti iliyokusanywa inaingia kwenye akaunti rasmi ya Halmashauri kwa wakati.” alisema Mhagama.
Aidha, Mhagama alitoa onya kali kwa watendaji wanaochelewesha kuwasilisha fedha zilizokusanywa au kutumia mapato kwa matumizi yasiyoruhusiwa, akibainisha kuwa hatua za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maagizo hayo.
“Hakutakuwa na huruma kwa mtumishi yeyote atakayebainika kutumia vibaya fedha za serikali au kuchelewesha kuziwasilisha. Halmashauri haitasita kuchukua hatua kali, ikiwemo kuwasilisha suala hilo katika vyombo vya uchunguzi.” aliongeza Mhagama.
Katika kikao hicho, washiriki walipata fursa ya kujadili changamoto zinazokabili ukusanyaji wa mapato, ikiwemo elimu ya ujazaji wa taarifa za ukusanyaji wa mapato kwenye mfumo wa FASS, ucheleweshaji wa baadhi ya makusanyo kutoka vyanzo vya ndani, pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi na ada.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Ndugu Seif Issa , Mtendaji wa Kijiji cha Sango, alisema kikao hicho kimekuwa muhimu kwani kimetoa mwongozo wa wazi juu ya namna bora ya kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa njia za kidijitali na kuongeza uwazi katika matumizi.