
10/05/2025
JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema hivi karibuni wakati likiendelea na uchunguzi wa tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa kwa Mfuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mpaluka Said Nyagali maarufu Mdude na watu wasiofahamika na kisha kutoweka naye kusikojulikana, wamejitokeza baadhi ya watu na viongozi wa CHADEMA na kutoa matamko mbalimbali ikiwemo kutaja baadhi ya majina ya Askari wakiwatuhumu kuhusika na tukio hilo bila kuwasilisha ushahidi wowote.
Kupitia taarifa ya leo Mei 10, 2025 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga Jeshi hilo limetoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote cha watu wenye nia ovu kutojaribu wala kuthubutu kujihusisha na uhalifu wa aina yoyote ikiwemo kudhuru Askari ama familia za Askari.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeeleza kuwa kabla ya mtu au kikundi cha watu kufikiria kufanya hivyo, wajionye sana na wasifikiri kufanya kitendo hicho ni rahisi kwao huku likisisitiza kuwa halitasita kumchukulia hatua za kisheria na kumshughulikia mtu au kikundi chochote cha watu watakaojaribu kufanya uhalifu kutokana na matamko au kauli hizo zinazotolewa.