09/05/2025
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wazazi nchini kuzingatia malezi na makuzi bora ya watoto tangu kipindi cha mimba hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka 18.
Dkt. Gwajima amesema hayo Mei 08, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia itakayofanyika Mei 15, 2025.
Waziri Dkt. Gwajima amesema majukumu ya familia ni mengi lakini kubwa ni kutoa huduma ili kukidhi mahitaji ya watoto na familia sambamba na kusimamia malezi na makuzi mema ya watoto. Aidha, amesema familia ina jukumu la kurithisha mila na tamaduni nzuri kwa watoto na familia kwa ujumla kizazi hadi kizazi.
Ameongeza kwamba Taifa lolote lenye maendeleo endelevu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hutokana na namna ambavyo watoto wamelelewa na kukuzwa kwa kuzingatia misingi ya malezi chanya inayoendana na maadili, mila na desturi njema za kitanzania.
Waziri Dkt. Gwajima amewahimiza Wazazi na Walezi kutimiza wajibu wao wa malezi na matunzo ya watoto ili kumkuza mtoto kuwa na tija kwa familia na taifa kwa ujumla ili kufanikisha hilo amewaomba wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao mara kwa mara ili kuimarisha muunganiko (bond) baina ya mzazi na mtoto hasa kwa kuwekeza nguvu nyingi zaidi za malezi kwenye umri wa chini ya miaka 8 kipindi ambapo, ubongo unakua kwa asilimia 90.
Pia amewataka wazazi na walezi kujua maendeleo ya mtoto na changamoto zinazomkabili kwa wakati na kuzipatia ufumbuzi kabla hazijaleta madhara makubwa.
Akieleza jitihada za Serikali kupitia Wizara anayoisimamia kuwa inaendelea kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho ya Sheria Tatu ambazo ni Sheria ya Mtoto, Sura ya 13, Sheria ya Makosa ya Kimtandao, Sura ya 443, na Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21 huku marekebisho hayo yakilenga kuondoa upungufu unaojitokeza katika utekelezaji wa masharti katika sheria husika ili kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto.