13/03/2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dkt. Zarau Kibwe, amepongeza uongozi wa Rais akieleza kuwa ni chanzo cha kuongezeka kwa kiwango cha mkopo ambacho Tanzania inaweza kupata kutoka Benki ya Dunia, kutoka Dola bilioni 5 (zaidi ya Shilingi trilioni 10) hadi Dola bilioni 12 za Marekani (zaidi ya Shilingi trilioni 25).
"Sijui huko nyumbani k**a mnaliona au kulizungumza hili. Katika muda mfupi ambao Rais Samia ameingia madarakani, ukomo wa Tanzania kwenye uhusiano wake na Benki ya Dunia umeongezeka kutoka dola bilioni tano hadi bilioni 12. Hili si jambo la kawaida," amesema Kibwe.
Kwa upande wake, Waziri Ulega amempongeza Kibwe kwa kushika wadhifa huo mkubwa k**a Mtanzania, akisema kuwa Watanzania wanajivunia mafanikio yake. Pia, ametumia fursa hiyo kueleza maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, ikiwemo ujenzi wa barabara, mwendokasi na madaraja.
Ulega amegusia changamoto ya wakandarasi wa kigeni kuchelewesha miradi, akipendekeza kwamba wanapaswa kufungua akaunti Tanzania ili kuwezesha malipo kufanyika haraka na miradi isikwame.
Katika majibu yake, Kibwe amemhakikishia Waziri Ulega kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku akimpongeza kwa msukumo mkubwa katika sekta ya ujenzi.
"Niliona mabadiliko makubwa Dar es Salaam na nikaambiwa ‘there is a new sheriff in town’. Hongera sana kwa kazi nzuri, mambo yako yanaonekana," amesema Kibwe.
Benki ya Dunia pia imethibitisha kuunga mkono mradi mkubwa wa barabara kuelekea Kusini mwa Tanzania, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Mzinga eneo la Kongowe, Dar es Salaam.
Kibwe ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika inayohusisha takribani nchi 23. Mtanzania wa kwanza alikuwa Christopher Kahangi aliyeshika wadhifa huo kati ya mwaka 1968 hadi mwaka 1970.