
15/09/2025
Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred amewaomba waendesha maghala waache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia maadili na uadilifu.
Amesema hayo Septemba 12,2025 kwenye mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa ubora wa korosho ghafi yaliyowakutanisha wadau mbalimbali wa zao hilo, kwa lengo la kuzidi kulipa thamani ambapo amewasisitiza waendesha maghala wasifanye kazi kwa mazoea.
Ameongeza kuwa ili kuendelea kubaki vinara kwenye sekta ya zao la korosho ni wajibu wa kila mtu katika kitengo chake kuhakikisha anasimamia ubora wa zao hilo, ikiwemo wasimamizi wa maghala kupokea korosho zenye ubora.
“Tunachopigania sisi hapa ni nchi, hatupiganii mtu mmoja bali maslahi ya taifa. Tukipeleka korosho yenye ubora wa hali ya juu, inamaanisha tutaendelea kupata wanunuzi wengi kupitia Tanzania, kuimarisha ushindani, bei zitapanda na wakulima watanufaika.” Amesema Alfred.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara Wakili Richard Mwalingo, amesema serikali haitaweza kumvumilia mtu yeyote atakayehusika na kuhujumu ubora wa korosho.
Ameongeza kuwa korosho ni moja ya mazao ya kimkakati nchini Tanzania hivyo amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuweka uzalendo mbele kwa kusimamia kanuni na maelekezo wanayopewa katika kutekeleza majukumu yao.
Aidha, ametoa maelekezo kwa washiriki kuhakikisha wanawafikishia wakulima elimu waliyoipata huku akiiahidi Bodi ya Korosho kuwa mamlaka za mkoa na wilaya ziko tayari kushirikiana ili kuhakikisha miongozo inatekelezwa kwa lengo la kufikia malengo ya uzalishaji wa tani milioni 1 ifikapo mwaka 2030.
Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo ikiwemo Nyaburuma Wanjara, wamesema mafunzo hayo yamewakumbusha kusimamia kanuni ili kuhakikisha ubora wa korosho unakuwa juu na kufanya pato la taifa kuzidi kukuwa.